The House of Favourite Newspapers

Acha Mitungi, Nani Kakuambia Huo ni Ujanja?

0

Drink-Menu-BackgroundKuna makala kama mbili hivi niliwahi kuandika na kueleza jinsi baadhi ya watu wanavyotumia pesa zao nyingi kwenye ulevi huku wakiishia kwenye matatizo na faida kwa kunywa kilevi hicho ikiwa hakuna.

Nawajua watu wengi huko mtaani baadhi wakiwa ni marafiki, ndugu na majirani zangu ambao walikuwa wakishindana kwa kutafuta heshima baa, lakini baada ya kuona wamebugi sasa wanatamani kuacha lakini inakuwa ngumu.

Ninayo mifano ya watu ambao walidiriki kufunga ili kumuomba Mungu awasaidie watoke kwenye unywaji wa pombe lakini huwezi kuamini mpaka leo watu hao pombe na wao, wao na pombe.

Katika mazingira hayo unaweza ukawa unajiuliza kwa nini baadhi ya watu wanakunywa pombe lakini moyoni wanatamani kuacha lakini wanashindwa? Kuna siri gani katika hili?

Labda kama ulikuwa hujui, nikujuze tu kwamba, wapo watu wengi ambao baada ya kuwa kwenye ulevi na ukawasababishia matatizo kwenye familia, kuwaathiri kiafya na hata kuwafanya wakaachishwa kazi, walikaa chini na kuamua kwa dhati kabisa kujitoa kwenye starehe hiyo.

Miongoni mwao walifanikiwa licha ya kwamba ilichukua muda kidogo. Ni lazima ichukue muda kwa sababu kuacha pombe, sigara au uzinzi huwezi kuamka tu na kusema ‘kuanzia leo basi’.

Lazima kwanza ufanye majadiliano na moyo wako, ukubali kuacha kisha na wewe uchukue hatua ambazo zitakufanya utimize lengo hilo.

Hivyo basi, kabla ya kuchukua uamuzi wa kuacha pombe, kwanza jiulize kwa nini unataka kuacha? Andika sababu hizo na uoneshe kutamani kufanikiwa.

Sababu hizo lazima ziwe zile za kukera na kukufanya ukose heshima mbele ya jamii, kama vile kulewa na kulala mitaroni, kupoteza pesa nyingi, kukabiliwa na hatari ya kupata magonjwa, kumpiga mkeo, kuachishwa kazi na nyingine za kufanana na hizo.

Endapo unakumbana na moja ya matatizo hayo au yote, ukikaa chini utaona umuhimu wa kuacha. Hivi huwaoni wale ambao mpaka leo wanafanya kazi za maana lakini maisha yao hayana mbele wala nyuma?

Nikueleze tu kwamba, pombe haikuwahi kuwa na faida kwa mwanadamu. Sanasana ukimuuliza mtu sababu ya kunywa pombe atakuambia eti inaondoa stresi! Jamani hivi pombe inaondoa stresi au inazipumzisha tu?

Haya, mwingine atakuambia anakunywa pombe kwa sababu ni starehe kama zilivyo starehe nyingine. Hivi ni starehe gani hii ambayo inakulazimu utumie pesa ambayo ungeweza kuitumia kwenye mambo ya kimaendeleo?

Ni starehe gani ambayo inakufanya unakuwa mzembe kazini, unatibuana na mkeo kila siku, unaishia polisi, unabania pesa kwa ajili ya pombe wakati watoto wako wanakosa huduma za msingi?

Ninapofika hapo ndipo napata ile nguvu ya kuwashawishi wanaokunywa pombe kuacha. Nikuambie tu wewe unayeendekeza pombe kwamba, siku ukiamua kuacha utaona mabadiliko makubwa sana kwenye maisha yako.

Unajua itakuwaje? Kwanza pesa zako ambazo unazipata kwa shida utazielekeza kwenye mambo ya kimaendeleo, pili yawezekana pombe ilikuwa inakufanya unakuwa mbali na familia yako, sasa utakuwa karibu nayo kwa sababu huwezi kuchelewa kurudi nyumbani.

Tatu, wapo waliodhoofika kwa sababu ya pombe, ukiacha utaona utakavyonawiri. Lakini nne utakuwa umeenda sambamba na maamrisho ya dini yanayokataza unywaji wa pombe.

Kwa kumalizia niseme tu kwamba, kunywa pombe wala siyo ujanja hivyo kama hujawahi wala usifikirie. Kama unakunywa wala sikushauri unywe kistaarabu, ipe kisogo kabisa kwa sababu mwisho wa yote inaweza kukupotezea heshima yako.

KUNUNUA NA KUSOMA MAGAZETI YA GLOBAL PUBLISHERS ONLINE, INGIA HAPA==>VODACOM M-PAPER APP

*********

JIUNGE NA SOCIAL MEDIA ZETU:

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA

INSTAGRAM: @Globalpublishers

ERIC SHIGONGO INSTAGRAM: @ericshigongo

TWITTER: @GlobalHabari

FACEBOOK: @GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers

GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE: @shigongotz

Leave A Reply