The House of Favourite Newspapers

Achana na Mambo ya Kitoto, Ingia Kwenye Majukumu ya Mtu Mzima!

0

RAFIKI yangu, wewe ni mwenye ushawishi. Una muda mwingi wa kufanikiwa. Hata pale unaposhindwa, unaweza kuanza tena na kufanikiwa, maana huna cha kupoteza.

Jenga nidhamu ya matumizi mazuri ya pesa yako, mawasiliano, fanya unachokipenda na ikiwezekana tembelea maeneo mbalimbali ili kupanua uelewa wako.

Ukifikisha umri wa miaka 30, ni kipindi cha mabadiliko kwenye maisha ya mtu na taaluma yake. Ni kipindi ambacho malengo ya wengi kitaaluma na familia huanza kuwa wazi na shauku ya kufika sehemu fulani kimaendeleo huongezeka zaidi.

Vijana wengi hasa wa kiume huwaza kutoka nyumbani na kuanza maisha binafsi ili kujiandaa kujenga familia. Kwa lugha nyingine ni muda wa kuachana na mambo ya kitoto na kuingia kwenye majukumu ya mtu mzima.

Katika mazingira kama haya, unatakiwa kufanya nini ili kufanikisha safari yako ya mafanikio?

Kadiri unavyokua katika taaluma yako, kabla hujafika miaka 30, unatakiwa kujifunza siyo tu kwa wale waliokuzidi, bali hata kutoka kwa wale ulionao kwenye ngazi moja.

Hii itakuhakikishia ujenzi wa msingi wa maisha kwa sababu utapata mbinu nyingi za kuzikabili changamoto zinazoweza kuibuka wakati ukitekeleza mipango yako. Wao watakufunza uzoefu walionao katika maisha ambao unaweza kuwa msaada kwako.

Uzoefu pia unaweza kuupata kutoka kwa watu waliofanikiwa kimaisha kama wafanyabiashara wakubwa. Jitahidi kufanya kazi sehemu mbalimbali ikiwemo viwandani au kwenye shule hata kama ni kazi za muda mfupi au za saa chache.

Marafiki na watu wenye mawazo yanayolingana na mipango yako, watakusaidia kufanikisha ndoto zako.

Kuwa na nidhamu katika matumizi yako ya pesa, weka bajeti na hakikisha unaifuata. Acha kutumia pesa yoyote unayoipata bila mipango.

Jifunze kuweka akiba na utoke nyumbani kwenda kujitegemea. Hakikisha unalipa madeni yote unayodaiwa mapema mara upatapo pesa ili kuzuia yasikuandame kiasi cha kushindwa kulipika.

Kama hutaki kuajiriwa, lakini unataka kufanya biashara, jitahidi uanze kuifanya kabla hujaoa au kuolewa. Utakuwa muoga sana na hutakuwa na uthubutu wa kutosha pale tu utakapoanza kuwa na familia na maendeleo ni ya muhimu kuanzia mwanzo wa taaluma yako.

Jitahidi kadiri uwezavyo uanzishe biashara hata kama ni ndogo kwa sababu utakapoweza kujifunza mbinu hizi mapema utajifunza namna ya kupata hasara kwa gharama ndogo.

Kumbuka msingi mzuri wa ujuzi wa biashara na pesa utakusaidia kufanikiwa baadaye.

Unachopaswa kufanya ni kujenga tabia njema na maadili mazuri; tabia inajengwa kuanzia kwenye matumizi mazuri ya muda, maadili ya kazi, kujiwekea mipaka ya kazi au maisha, mazoezi, kula vizuri au kuwa na nidhamu na pesa zako binafsi.

Jifunze kukabiliana na kupanda na kushuka kimaisha. Maisha ndiyo hayahaya, wasikilize wakubwa katika kujijenga vyema kimaadili.

Jitahidi kujenga mawasiliano yako na watu muhimu unaokutana nao katika shughuli mbalimbali za kikazi au biashara. Mawasiliano ni muhimu maana hujui ni wakati gani utahitaji msaada kutoka kwa mtu fulani.

Zaidi sana, tafuta marafiki wenye tija kwako na hakikisha unawasiliana nao mara kwa mara ili kutengeneza mtandao mzuri wa maendeleo.

Lakini mawasiliano ni pamoja na ujuzi wa mazungumzo na kuzungumza mbele za watu kwa kujiamini na ujasiri na kabla ya kuzungumza, fikiria kwanza na fahamu kwa undani unachokisema.

Wekeza nguvu katika kujenga mawasiliano imara na endelevu na watu wa karibu yako ambao watakusaidia kufanikiwa zaidi.

Kingine cha muhimu kwako ni kufanya unachokipenda. Kila mtu anajua amekuja kufuata nini hapa duniani. Tambua kile unachokipenda na lenga kuwa bora kwenye hicho unachokifanya kwa kupenda kujifunza zaidi kwa vitendo.

Tafuta mtu ambaye amewahi kupita kwenye njia unayotamani kupita. Kuwa mbunifu, mwaminifu na heshimu muda unaoutumia pamoja naye kwa sababu anajifunza kutoka kwako pia.

Kadiri umri unavyoongezeka, ndivyo sababu za kutokufanya jambo fulani huongezeka na mwisho wa siku utakuja kujuta kwa kutokujaribu au kuanza mapema.

Nakutakia mafanikio kwenye maisha yako, tukutane wiki ijayo. Kwa ushauri, nitafute kwenye namba hiyo hapo juu.

Leave A Reply