Achana Na Ubize Usio Na Maana, Tenga Muda Wa Kuwa Naye

NI Ijumaa nyingine tu­napokutana katika uwanja wetu huu mzu­ri, tukijuzana na kuelimishana kuhusu mambo mbalimbali ya­husuyo mapenzi. Mada yetu ya leo ni kama inavyojieleza hapo juu.

 

Je, mara ya mwisho kwa wewe na mpenzi wako kupata muda wa kukaa pamoja au kutoka ‘out’ ilikuwa ni lini? Una desturi ya kutoka na umpendaye, mkaenda mahali tulivu ambapo mtapata muda wa kujadiliana na kubadil­ishana mawazo kuhusu maisha na mapenzi? Kama jibu lako ni hapana, unaishi kwenye mapen­zi yaliyokosa uhai.

 

Maisha yanaenda kasi sana, wanandoa wengi au watu am­bao wapo kwenye uhusiano wa kimapenzi, wanajikuta wakikosa kabisa nafasi ya kuwa pamoja kutokana na kila mmoja kuweka kipaumbele katika kazi, biashara au shughuli nyingine za utafutaji pesa au malezi ya watoto.

 

Matokeo yake, watu wengi wanaishi kwa mazoea tu lakini katika uhalisia, mapenzi yana­kuwa yamepungua sana au hayapo kabisa.

Watafiti wa mapenzi wanaeleza kwamba hakuna kazi ngumu kama kuishi pamoja wewe na mpenzi wako, iwe ni kwenye ndoa au uhusiano wa kawaida wa kimapenzi kwani ni rahisi sana watu kuchokana. Hata kama unampenda vipi, lazima kuna muda utamchoka au utachoshwa na mazin­gira ambayo mmekuwa mkiishi siku zote.

 

Unapofikia hatua hii, kitu pekee kinachoweza ku-refresh akili na hisia zako, ni wewe na umpen­daye kutoka pamoja na kwenda sehemu tofauti kama ufukweni, hotelini au sehemu yoyote tulivu ambayo mtakaa pamoja, mtakunywa au kula na kufurahi. Kitendo hiki kinata­jwa kuwa siri kuu ya kufufua mapenzi na kuondoa ile hali ya kuchokana.

 

Haijalishi umeishi kwa muda gani na mpenzi wako, hata kama mna miaka kibao, lazima muendelee kutoana out mara kwa mara. Hata kama tayari mmeshazaa watoto na wamekuwa wakubwa, suala la out halikwepeki kama mnataka kuishi kwa amani na upendo. Wengi wanaamini kwamba mpenzi mpya pekee ndiye anayetakiwa kutolewa ‘out’, jambo ambalo siyo sahihi.

 

Mkirudi, kila mmoja atashangaa kwamba mapenzi yake kwa mwen­zake, yatazidi ma­radufu, kama kulikuwa na migogoro ya hapa na pale, itaisha na mtaen­delea kuishi kwa amani na furaha.

 

Wengi tu­nasumbuliwa na kasumba kwamba ili kumtoa mpenzi wako out, ni lazima waleti yako iwe imejaa, lazima mkatumie fedha nyingi au lazima umpe­leke sehemu ya gharama. La hasha, siyo lazima kabisa.

 

Kwa mfano, inakugharimu nini wewe na mpenzi wako kutoka na kwenda ufuk­weni, mkaagiza soda, maji au vinywaji mnavyovipenda, mkakaa kwenye mchanga wa bahari na kupunga up­epo mwanana?

 

Hata kama hakuna ufukwe hapo mnapoishi, mnaweza kutoka na kwenda sehemu yoyote tulivu, iwe ni kwenye uwanja wa mpira muda ambao hakuna watu, sehemu za milimani au mahali popote ambapo mtakuwa wawili tu, inatosha kabisa. Unaweza kununua matunda, vinywaji au vitafunwa mnavyovipenda, mkaenda navyo mpaka sehemu mliyoichagua, siyo lazima uwe na fedha nyingi.

 

Ili mtoko wako na umpen­daye ukamilike, kuchagua sehemu ya kwenda ni jam­bo la kwanza lakini kubwa zaidi, lazima ujue kwamba mkiwa ‘out’, unapaswa kufanya nini ili mpenzi wako afurahi na kufufua upya hisia za mapenzi ndani ya moyo wake.

Ni matumaini yangu kwamba utakuwa umejifun­za kitu kikubwa na nakuhak­ikishia kwamba ukiyafanyia kazi haya, utayafurahia mapenzi.

Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri, kwa maoni, ushauri, nicheki kwa namba za hapo juu.

Facebook: Hash Power
Insta: Hashpower 7113
Mapenzi & Uhusiano WhatsApp: 0719 401 968

Toa comment