The House of Favourite Newspapers

ACT: Bila sera za kitaifa, Magufuli hatafika popote

0

5rr96pRGKatibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo,Samson Mwigamba.

Na Boniphace Ngumije

KATIBU Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo,Samson Mwigamba amesema bila Rais John Magufuli kuhakikisha serikali yake inakuwa na sera za kitaifa ambazo zitaisaidia kuwa dira katika kuleta mabadiliko aliyoyaahidi wakati wa kampeni zake, kasi ya utendaji aliyonayo kwa sasa haitafika popote.

Akizungumza na gazeti hili mwanzoni mwa wiki hii,Mwigamba alipongeza utendaji wa Dk. Magufuli alioanza nao katika kutekeleza majukumu yake na kuongeza kuwa jambo
ambalo litamfelisha litakuwa hilo la sera za kitaifa ikiwa tu atashindwa kuunda mikakati ya kuhakikisha zinapatikana mapema.

Alisema katika zama hizi za ukomavu wa demokrasia duniani ni kosa kubwa kwa sera za kuisaidia nchi kujengwa na chama kimoja cha siasa hata ikiwa ndicho hicho kinachoshikilia dola.

Mwigamba aliendelea kusema, kwa kuwa uchaguzi ulifanyika na kumalizika salama hatimaye kutoa mshindi ambaye chama chake kinaamini alishinda kwa haki kutokana na upepo wa kisiasa ulivyokuwa, rais anatakiwa kuhakikisha anavishirikisha vyama vyote vya siasa kuunda sera ili kuvifanya navyo vishiriki katika maendeleo ya kitaifa jambo ambalo litakuwa msingi bora pia kwa kipindi kijacho hata ikiwa chama pinzani kitashika dola.

Aidha, katibu mkuu huyo alimpa pongezi Dk. Magufuli kwa niaba ya chama chake kutokana na uwepo wa asilimia 60 ya vipaumbele vilivyomo kwenye ilani ya chama chake kwenye hotuba aliyoisoma wakati analifungua Bunge kwa mara ya kwanza Ijumaa iliyopita.

“Rais amefanya kitu kizuri kuipitia ilani ambayo mgombea wetu wa urais, Anna Mghirwa alimpa siku anakabidhiwa cheti cha ushindi wa urais na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva pale kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, nina uhakika mkubwa ilani yetu imempa dira nzuri hata kuona umuhimu wa  uorodheshwa kwa wingi vipaumbele vyetu kwenye hotuba yake,” alisema Mwigamba.

Leave A Reply