ACT Wazalendo Yalitaka Jeshi La Polisi Liwaachie Viongozi Wa Chadema
Chama cha ACT Wazalendo kimetoa wito kwa Jeshi la Polisi Tanzania kuwaachia huru viongozi waandamizi wa CHADEMA waliokamatwa, akiwemo Mwenyekiti Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti Tundu Lissu, pamoja na wanachama wengine.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu, viongozi hao walikuwa wakijiandaa kutekeleza haki yao ya kikatiba ya kuandamana walipokamatwa, hatua ambayo chama hicho kimeilaani kwa nguvu zote.
“Tunalitaka Jeshi la Polisi kuwaachia huru bila masharti viongozi wote wa CHADEMA waliokamatwa kwa sababu maandamano ni haki ya kikatiba,” amesema Dorothy Semu.
Taarifa hiyo pia imetoa wito kwa Serikali kuanzisha mazungumzo ya kina na dhati, ambayo yatashirikisha vyama vya siasa, Jeshi la Polisi, viongozi wa dini, na wadau wa demokrasia kwa ujumla. Semu amesisitiza kuwa mazungumzo hayo yanahitajika ili kushughulikia na kupata ufumbuzi wa utekaji na mauaji ya raia, ambayo yalikuwa sababu ya maandamano hayo.
ACT Wazalendo imeeleza kuwa inafanya jitihada za kuzungumza na viongozi wa Jeshi la Polisi, CHADEMA, CCM, na Serikali kwa ujumla, kwa lengo la kutafuta suluhisho kwa njia ya haki, hekima, na kwa kuzingatia maslahi mapana ya taifa.