The House of Favourite Newspapers

ADAIWA KUMCHOMA VISU MWENZAKE, AMSUBIRIA AFE!

UKIULIZWA ‘Kwa nini umemchoma kisu mwenzio na kumuua?’ Na ukagundua kuwa kosa lake lilikuwa ni kuvaa raba zako nyeusi za elfu kumi; majuto yake baada ya tukio ni makubwa kwani kesi yake ni nzito, Uwazi lina kisa kizima.  

 

Rashidi Mustapha (48), mkulima na mkazi wa kijiji na Kata ya Nyihogo, wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga yuko kwenye majuto baada ya kukamatwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kumchoma kisu na kumsababishia kifo Daniel Mtambala (30).

 

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo lililotokea Jumamosi iliyopita ambao hawakupenda majina yao kuandikwa gazetini walisema, watu hao walianza kugombea viatu aina ya raba nyeusi ambapo kila mmoja alidai ni vyake.

 

“Sisi hatukuweza kujua nani mkweli kwa sababu tulikuta wananyang’anyana viatu, raba nyeusi, kila mmoja akidai ni vyake,” mmoja wa mashuhuda alisema bila kufafanua kama watu hao walikuwa wakifahamiana au la!

 

Kama wasemavyo Waswahili; chachu kidogo huchachua donge zima ndivyo ilivyokuwa mara baada ya mabishano ya ‘raba zangu’ amani ikatoweka kwa wawili hao kuanza ugomvi. Ghafla eneo la tukio liligeuka kuwa jekundu baada ya Mustapha kudaiwa  kumchoma visu Mtambala. Inaelezwa kwamba hata baada ya marehemu kuchomwa visu hakuacha kupambana na mtuhumiwa bali aliendelea kupigania viatu huku damu nyingi zikimtoka.

 

Kuvuja damu kulipozidi mashuhuda wanasema marehemu alionekana kuishiwa nguvu huku mtuhumiwa naye akionekana kuchoka. Inadaiwa kuwa mashuhuda walikwenda kuwaamulia na kupiga simu polisi ambao walifika na kuwachukua mtuhumiwa na majeruhi.

 

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Richard Abwao amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa, lilitokea Jumamosi majira ya saa kumi na mbili jioni katika eneo la Nyihogo Transfoma.

“Ni kweli chanzo cha tukio hilo ni ugomvi uliotokana na kugombea viatu aina ya raba nyeusi na mbinu aliyotumia Rashid Mustapha ni kumchoma visu mkono wa kushoto mwenzake, Daniel Mtambala na kumfanya atokwe na damu nyingi, alipofikishwa hospitali mauti yalimfika,” alisema Kamanda Abwao.

 

Mwili wa marehemu Mtambala umehifadhiwa katika Hospitali ya Mji wa Kahama na kwamba kisu ambacho kilitumika kwenye mauaji hayo kimechukuliwa na polisi kama kielelezo, ambapo mtuhumiwa anadaiwa kukiri kosa na kwamba atafikishwa mahakani baada ya upelelezi kukamilika.

 

Hata hivyo, Kamanda Abwao alitoa rai kwa wananchi kwa kusema: “Nawaomba wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na kama kutatokea tafrani ya uvunjifu wa amani ni bora wakatoa taarifa katika vyombo ya kisheria ili kuangalia namna ya kulitatua tatizo.” Hadi tunakwenda mitamboni, marehemu alikuwa bado hajazikwa

Comments are closed.