The House of Favourite Newspapers

Adamu Kuambiana Ashtuka Ray Kuzaa na Chuchu Hans

0
Chuchu Hans na mtoto wake.

MPENZI msomaji, hii ni kolamu mpya ya kiburudani lakini ndani yake kuna ujumbe wenye kugusa jamii. Ni kona ya kufikirika.

Wapo watu ambao walishatangulia mbele ya haki lakini endapo kama wangekuwa hai kuna vitu vikubwa zaidi wangeweza kufanya. Mwandishi anavaa uhalisia wa wahusika na kubashiri baadhi ya mambo ambayo wangependa kuyajua na kuyafanya hapa duniani. Maswali na majibu ni ya kutunga, lakini lengo ni lilelile. Kufikisha ujumbe katika staili ya kiburudani.

Wiki iliyopita tulianza na marehemu Amina Chifupa na leo ndoto ya mwandishi imemkutanisha na aliyekuwa gwiji mkubwa wa filamu za Kibongo, Adam Philip Kuambiana ambaye alifariki miaka mitatu iliyopita baada ya kuugua ghafla. Twende pamoja…

Muziki laini unasikika kwa mbali lakini maneno yake yanaeleweka. Nashindwa kabisa kujua ni wimbo gani au umeimbwa na nani lakini unaburudisha sana na hapohapo najikuta nikitikisa kichwa kuendana na ‘biti’ ya wimbo.

Mbele kuna watu wengi, ingawa wanajionesha kwangu lakini nashindwa kuwatambua ni akina nani na wapo hapo kwa lengo gani.

Wakati nawaza hayo, ghafla nasikia mluzi ulioambatana na kutajwa kwa jina langu, najiuliza ni nani huyo na hapa niko wapi? Lakini sikupata nafasi ya kung’amua jibu, haraka sana anakuja mtu anayenifanya nibaki namshangaa.

Ray na Chuchu Hans.

Yes, ni Adam Kuambiana akiwa amevaa pensi na tisheti nyeusi, kichwani nywele zikiwa na dawa yenye rangi ya njano, mkononi ameshika chupa yenye kinywaji kikali sana, hata hivyo namkazia macho na kungundua kwamba anayumba na maneno yake hayatoki sawasawa.

Kuambiana: Oya, habari za miaka? Umefikaje huku?

Mimi: Salama kaka, kabla ya yote naomba unieleze ukweli hapa ni wapi na wewe unafanya nini?

Kuambiana: Nitakuambia baadaye, vipi huko mambo yakoje?

Mimi: Salama tu, hivi uliondokaje kaka?

Kuambiana: Nakumbuka nilikuwa naandaa filamu yangu na kambi ilikuwa Sinza, siku hiyo nilikuwa nakunywa kama hivi (akinyanyua chupa yake), ghafla nilianza kusikia tumbo likiniuma sana na kuanzia hapo sikujua tena kilichoendelea hadi nilipojikuta niko huku niliko, lakini karibu sana na wewe.

Mimi: Sikaribii chochote, nahisi leo nimekuja kutembea tu. Wengine wako wapi?

Kuambiana: Recho alikuwa hospitali, mwanaye anasumbuliwa na homa kidogo, utamuona muda siyo mrefu sana. Kanumba yuko lokesheni kuna filamu moja anaandaa na yule John Stephano unamkumbuka? Yeye ndiyo mkuu wa kanda yetu hii.

Mimi: Namkumbuka, ni kitu gani unakijutia sana kwamba hukukifanya wakati ukiwa kwenye ulimwengu wa sinema?

Kuambiana: Kuchezea muda. Nilikuwa na uwezo wa kufanya chochote kikubwa kutokana na ujuzi wangu wa filamu. Najua kuigiza, kuongoza na hata kuandaa stori nzuri ya filamu, lakini yote hayo sikuyafanya kwa sababu ya kuendekeza mambo yasiyokuwa ya msingi, najutia sana.

Mimi: Ni mambo gani ambayo yalikuhadaa na kushindwa kufanya vyema?

Kuambiana: Bwana eeeh. Ujana una mambo mengi.

Adam Kuambiana.

Mimi: Pole sana. Ni jambo gani liliwahi kukupa wakati mgumu kipindi uko kwenye ulimwengu halisi?

Kuambiana: Ugomvi wa Kanumba na Ray, kipindi kile hawaongei kisa magari. Niliwapenda wote na nilizoea kuwa nao pamoja kila mahali, sasa wakati wanatofautiana nilikuwepo pale Leaders na nikaanza jitihada za kuwapatanisha lakini ilikuwa kazi ngumu sana.

Mimi: Kwa sasa filamu zinapoteza msisimko na wasanii wengi wakubwa wameshaanza kuigiza tamthiliya, akiwemo JB wewe ungekuwepo ungefanya nini kuhakikisha soko linasimama kama ilivyokuwa huko awali?

Kuambiana: Utunzi wa stori nzuri, mandhari nzuri ya kuigizia na wasanii kuvaa uhalisia wa matukio lakini kubwa sana ni mfumo wa usambazaji, hapo kuna shida kwamba msambazaji mkubwa anakuwa mmoja ana-monopoly (anashikilia) soko na kuwalipa namna anavyojisikia.

Lakini kuna suala la nidhamu kwa wasanii matendo yao yaendane sawasawa na kazi yao ya kuelimisha jamii kupitia sanaa (anaendelea)…

Lazima wasanii wapende kazi yao na waache mzaha wakati wa kuandaa kazi. Nakumbuka niliwahi kuwachapa makofi Wema na Aunt Ezekiel pale Blue Mark Hotel baada ya kunizingua, ilikuwa ni filamu ya Saa Mbovu kama sikosei. Yote hayo ni kujitambua na kuthamini kazi yako.

Mimi: Hivi uliondoka bila mtoto?

Kuambiana: Hilo naomba nisilijibu kwa sababu nilikuwa na maisha mengine kabla ya sanaa kwa hiyo watu wajue tu kuhusu kazi yangu na hayo mengine nilishaachana nayo kwenye ulimwengu halisi. Vipi, Stara Thomas yupo?

Mimi: Yupo bwana, hajasimama sehemu moja maana leo utamsikia anafanya Bongo Fleva mara ghafla Gospo.

Kuambiana: Sawa, mfikishie salamu zangu. Mama Kanumba yupo? Lulu je? Kesi yake inaendeleaje? Ilishatolewa hukumu? Saguda wa Recho yupo? Kampuni yake na marehemu mkewe ipo? Ray na Johari bado wako pamoja? Uwoya je?

Mimi: Umeniuliza maswali mengi kwa wakati mmoja lakini nitakujibu. Mama Kanumba yupo. Lulu pia yupo. Kesi yao bado inaunguruma na mimi nikuombe tusiizungumzie, tuiachie mahakama. Saguda yupo kajaa tele. Kampuni yake na marehemu mkewe ya RASA ipo, Ray na Johari bado wapo ila kaka mkubwa siku hizi anaitwa baba, kazaa na Chuchu Hans.

Kuambiana: Brai (Brighton) acha utani bwana, Chuchu na Ray wapi kwa wapi? Chuchu si aliolewaga na mtu mwingine?

Mimi: Sasa huniamini ndugu yangu? Huo ndiyo ukweli. Kuhusu Uwoya yupo na siku hizi amejiingiza kwenye ujasiriamali, anamiliki baa pale Sinza, maisha yanaendelea kaka.

Kuambiana: Dah! Wewe bado upo Global? Hivi yule mwandishi Zungu (Shakoor Jongo) yupo? Musa Mateja je? Vipi akina Imelda Mtema na yule Erick Evarist ambaye mlikuwa mnapuyanga naye kutafuta stori? Usisahau kumsalimia bosi kubwa, Eric Shigongo maana ndiye alinifanya nianze kuigiza. Alipenda uwezo wangu wa kuzungumza Kingereza siku moja tulipokutana mwanzo, msalimie sana.

Mimi: Zimefika. Mimi bado nipo Global. Zungu kwa sasa hayupo Global. Mateja yupo lakini siku hizi amejikita sana kwenye habari za michezo. Imelda Mtema bado anang’ara kama kawaida. Erick Evarist yupo, ni mhariri wangu kwa sasa. Bado tunafanya kazi pamoja.

Kuambiana: Sawa Masalu, chukua namba zangu tutakuwa tunawasiliana kila mara. Najisikia kuchoka halafu nataka kwenda sehemu nina miadi na Sharo Milionea, muda nao unayoyoma.

Mimi: Sawa Kuambiana. Nitajie namba zako nitakupigia kila mara ili tuwe tunabadilishana mawazo. Napenda sana uwezo wa akili yako kuhusu maisha.

Kuambiana: Namba zangu ni 0713 65….

Wakati Kuambiana akitaja namba zake, ghafla nashtuliwa na maumivu ya mgongo na hapohapo nafumbua macho na kujikuta nipo kitandani kwangu. Tayari ni saa kumi na mbili na nusu. Najiandaa kwenda kazini nisije nikachelewa na kukutana na adhabu ya Saleh Ally, Mhariri Mtendaji wa ofisini kwetu na mtu anayependa kuona mambo yanasonga kwa weledi wa hali ya juu.

Kwa naoni na ushauri nicheki kwa namba hizi; 0673 42 38 45.

Makala: Brighton Masalu | AMANI|SAA 9 USIKU KITANDANI MWANGU!

Usipitwe na Matukio, Install App Yako ya Kijanja na Namba Moja Tanzania ya Global Publishers

Android ===>Google Play

iOS ===>Apple Store

==

Sanch: Mwanaume Lijali Anayemtaka Kimapenzi Awe Tayari Kufanya Hivi – Video

Leave A Reply