Wafanyabiashara waliopitisha makontena 349, kulipa faini ya mil 28.3 kila kontena

makontenaMamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewagomea kulipa kodi bila adhabu baadhi ya wamiliki wa makontena, ambayo yalitoroshwa kwenye bandari kavu bila kulipiwa kodi.
Badala yake, TRA imewapelekea hati ya malipo inayowataka wafanyabiashara hao, kuhakikisha wanalipa kodi hiyo na adhabu ndani ya siku saba, la sivyo watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.
Hatua hiyo inatokana na baadhi ya wamiliki wa makontena hayo, kuiomba TRA kuwasamehe kulipa adhabu waliyopewa badala yake waruhusiwe tu kulipa kodi stahiki ya Serikali.
Jumla ya makontena 349 yalitoroshwa katika bandari kavu bila kulipa kodi na kuikosesha Seri kali mapato ya Sh bilioni 80.
Wafanyabiashara hao, pia wameomba waruhusiwe kulipa kodi wanayotakiwa kulipa kidogo kidogo kwa madai kuwa wengine hawana uwezo wa kulipa kiasi hicho cha fedha kutokana na kutapeliwa na mawakala wao waliowatumia kwenda kulipa kodi hiyo.
Wakizungumza na wanahabari, baadhi ya wafanyabiashara hao walisema agizo la Dk Magufuli alilotoa Desemba 3, mwaka huu kuwa linawataka walipe kodi hiyo ndani ya siku saba.
Lakini wafanyabiashara walisema nyaraka za malipo walizopelekewa na TRA, zimewataka kulipa kodi na faini kwa pamoja wakati hizo siku saba alizotoa Dk Magufuli hazijamalizika.
Wafanyabiashara hao wanadai kuwa walishalipa kodi hiyo kupitia kwa wakala wao, kama taratibu za TRA zinavyowataka kuwatumia mawakala wa bandarini kulipa kodi, lakini kwa bahati mbaya wakala huyo hakufikisha kodi hiyo serikalini.
Walidai kuwa walifuatilia nyaraka za kodi kwa wakala wetu, lakini akawa anawaambia wasubiri.
“Tunaomba hii adhabu tusamehewe, kwani sio kosa letu ila tuko tayari kulipa kodi halali ya Serikali, lakini wakala wetu ndiye katuingiza kwenye matatizo haya na yeye tayari ameshatoroka,” aliongeza mfanyabiashara huyo.
Katika nyaraka za kodi ambazo TRA imewapelekea, kontena moja linatakiwa kulipiwa ushuru wa Sh milioni 40.5 ndani ya siku saba na adhabu ya Sh milioni 28.3. Hivyo jumla wanatakiwa kulipa Sh milioni 68.8 kama ushuru na adhabu.
Akizungumza na mwandishi kuhusu madai hayo ya wafanyabiashara, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa Walipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alisema adhabu walizoandikiwa wafanyabiashara hizo, wanatakiwa kuzilipa pamoja na kodi stahiki ndani ya siku saba.
Alisema wamewawekea adhabu hiyo kutokana na kitendo chao cha kuiibia Serikali na kwa taratibu za nchi, walitakiwa wawe mahabusu sasa hivi, lakini wametakiwa kulipa ushuru wa Serikali wakati wakiwa nje; hivyo wanastahili kulipa kiasi hicho cha fedha kama adhabu ya kukwepa kodi.
“Hawa walitakiwa kukamatwa na kuwekwa ndani, walitoa kontena nje ya utaratibu, adhabu hiyo ni ya kutoa makontena bila kulipa kodi,” alisema Kayombo. “Wakishindwa kulipa ndani ya muda huo tutawakamata tena na kuwafikisha mahakamani,” alieleza.
Kayombo alifafanua kuwa siku saba hizo walizopewa wafanyabiashara hao ni kusamehewa kutoshitakiwa mahakamani na sio kusamehewa kulipa adhabu wakati tayari walishakiuka taratibu.
Alisema wafanyabiashara hao, wachague kulipa ndani ya siku saba wasishitakiwe au waache ili wakutane na rungu la dola la kufikishwa mahakamani.
Alisema hadi sasa TRA imeshakusanya Sh bilioni 9.4 kati ya Sh bilioni 80 zinazotakiwa kulipwa kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara hao waliokwepa kodi.
CREDIT: MPEKUZI
Loading...

Toa comment