Afariki Dunia Baada ya Kuzidiwa na Pombe Kali!

Marehemu Bahati.

Na SAIMENI MGALULA | GAZETI LA IJUMAA| HABARI

MBEYA: Ama kweli pombe siyo chai! Kijana mmoja aliyetambulika kwa jina moja la Bahati anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 22 mkazi wa Kijiji cha Igawa Kata ya Lugelele Wilaya ya Mbarali mkoani hapa, amefariki dunia baada ya kuchanganya kunywa pombe za asili na konyagi.

Tukio hilo lililowafanya watu kushika tama, lilijiri juzi mchana katika kijiji hicho ambapo baadhi ya mashuhuda ambao hawakupenda majina yao kuandikwa gazetini walizungumzia kifo cha marehemu Bahati wakisema, kabla ya kufungua ofisi yake (duka la kuuza CD) alibeba chombo na kwenda kununua pombe ya asili aina ya ulanzi inayotokana na miti aina ya mianzi.

“Baada ya kununua alirudi na pombe hiyo hadi ofisini kwake na kufungua duka kisha kuanza kunywa, alikuwa akinywa kwa kasi, ikiisha anafuata tena na tena,” alidai shuhuda huyo. Shuhuda mwingine aliongeza kuwa, ilipofika jioni Bahati akabadili kinywaji na kuanza kunywa ‘konya’ mpaka kufikia mizinga minne ambayo ilimfanya aanze kutapika hadi pale wasamaria wema walipopiga simu kwa wazazi wake ambao ni walezi wanaomsimamia ndipo akakimbizwa katika Hospitali ya Serikali ya Rujewa kwa ajili ya matibabu.

“Baada ya kufikishwa hospitali, aliwekewa dripu ya maji lakini ilipoisha na kuongezewa ya pili kwa bahati mbaya akafariki dunia na maiti kuhifadhiwa mochwari kwa ajili ya taratibu za mazishi,” alizungumza shuhuda huyo.

Akilizungumzia tukio hilo mmoja wa ndugu wa marehemu, Peter Vicent alisema kuwa, alipigiwa simu mapema lakini alikuwa mbali kidogo ila alijitahidi kuwahi kwenda hospitali na kwa bahati mbaya alipofika Bahati alikuwa ameshafariki dunia. Akithibitisha tukio hilo, Diwani wa Kata ya Lugelele, Nelson Vicent  alisema kuwa, tukio hilo limetokana na kutokuwa na umakini katika matumizi ya pombe kali.

“Siyo kwa ubaya lakini nadhani hii itakuwa mfano kwa vijana ambao wanapenda kutumia pombe kali. Niliwahi kutoa wito kwa vijana kuachana na tabia za kufuata mikumbo kwa kutumia pombe kali,” alisema Vicent.

Marehemu alizikwa juzi katika Kijiji cha Mahongole Kata ya Imalisongwe wilayani Mbarali mkoani Mbeya.

Toa comment