The House of Favourite Newspapers
gunners X

AFCON 2025 Morocco: CAF Yatangaza Mamilioni kwa Bingwa na Washindi Wengine

0

Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) limetangaza rasmi muundo wa zawadi za fedha kwa ajili ya Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, itakayofanyika nchini Morocco na kushirikisha mataifa 24 kutoka barani Afrika.

Kwa mujibu wa muundo huo mpya, bingwa wa AFCON 2025 atajinyakulia kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 7, sawa na takribani Shilingi Bilioni 17.3 za Tanzania. Mshindi wa pili atapokea Dola Milioni 4 (takribani Shilingi Bilioni 9.96 za Tanzania).

Timu zitakazofanikiwa kufuzu hatua ya nusu fainali zitapokea Dola Milioni 2.5 kila moja, huku zile zitakazofika robo fainali zikipata Dola Milioni 1.3 kila timu.

Kwa upande wa timu zitakazomaliza safari yao katika hatua ya raundi ya 16, CAF imetenga zawadi ya Dola 800,000 kwa kila timu, sawa na takribani Shilingi Bilioni 1.98 za Tanzania.

Katika michuano hiyo, Tanzania (Taifa Stars) chini ya kocha Miguel Gamondi, itaanza kampeni yake kwa kibarua kigumu dhidi ya moja ya miamba wa soka barani Afrika, Nigeria. Mchezo huo umepangwa kuchezwa Desemba 23, kuanzia saa mbili na nusu usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Muundo huu mpya wa zawadi unaonesha dhamira ya CAF kuendelea kuongeza thamani ya michuano ya AFCON na kuzipa motisha kubwa zaidi timu shiriki, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona nani ataibuka bingwa wa bara hilo.

Leave A Reply