The House of Favourite Newspapers

Afisa Maliasili adaiwa kulishwa sumu

0

IMG-20160131-WA0007Marehemu Doris Olotu enzi za uhai wake.

Stori: Makongoro Oging’, UWAZI
ARUSHA: Ndugu wa Doris Olotu 47, (pichani)aliyefariki dunia Januari 2, mwaka huu katika Hospitali ya Misheni ya Selian jijini Arusha wamekuja juu na kudai kwamba, kifo cha ndugu yao huyo kilisababishwa na kulishwa sumu.

Kwa mujibu wa ndugu hao, kifo cha Doris aliyekuwa Afisa wa Wizara ya Maliasili na Utalii Shamba la Miti Meru-Arusha, Idara ya Utunzaji wa Kumbukumbu, kinahusishwa na tukio la kikazi kwa kudaiwa kuwa alikuwa akijua hujuma nzito.

“Unajua siku za nyuma kuliwahi kuripotiwa tukio la kupotea kwa nyaraka fulani kwenye ofisi ambayo marehemu alikuwa akifanyia kazi. Sasa inadaiwa kwamba hizo nyaraka hazikupotea bali ziliibwa na watu anaowajua yeye kwa manufaa yao.

IMG-20160131-WA0001Jeneza lillilobeba mwili wa marehemu likiombewa.

“Desemba 31, mwaka jana, wakaguzi wa hesabu za serikali walifika kwenye ofisi ya Doris kwa lengo la kukagua na ndipo alipobainika kupotea kwa nyaraka hizo muhimu kwa mahesabu. Wakawa wanamhoji kuhusu upotevu huo ambapo na yeye alionesha kumfahamu aliyekuwa nyuma ya tukio hilo.

“Tunasikiasikia kuwa, mtu aliyeiba hizo nyaraka anajulikana hata na baadhi ya wafanyakazi wenzake. Sasa alipopata taarifa kwamba wakaguzi wamekuja, akajua Doris akibanwa atamtaja, ndiyo akaandaa mpango wa kumuua kwa sumu,” alisema ndugu mmoja kwa sharti la kutotajwa jina gazetini.

Naye mfanyakazi mmoja wa maliasili aliyeomba kutoandikwa jina, aliyapa nguvu madai hayo na kueleza kuwa aliyehusika na wizi wa nyaraka hizo anajulikana na wafanyakazi wengi.

“Unajua sakata la kupotea kwa zile nyaraka liliwahi kuleta tafrani kubwa siku za nyuma. Kwa hiyo jamaa alivyosikia kuna wakaguzi wamekuja, akajua atatajwa, sasa ili kukwepa mkono wa sheria, akaandaa mpango wa kumuua,” alisema mfanyakazi huyo.

Rose Olotu ambaye ni mdogo wa marehemu, alisema kifo cha dada yake kimezua utata mkubwa katika ukoo kutokana na namna alivyofariki jambo ambalo hata taarifa fupi ya kifo chake iliyoandaliwa na ofisi aliyokuwa akifanyia kazi haikusomwa baada ya wanandugu kuikataa wakidai imejaa upotoshaji.

Alisema mmoja wa wafanyakazi ambaye alikuwa karibu naye siku ya tukio, aliponea chupuchupu kupigwa na akaondolewa msibani akituhumiwa alikuwa anajua kinachoendelea ndiyo maana hakutoa taarifa kuwa, Doris alinyweshwa sumu mpaka marehemu alipokuwa na hali mbaya hospitalini.

“Siku ambayo wakaguzi wa hesabu za serikali walifika ofisini kwake, marehemu hakurudi nyumbani. Inadaiwa eti aliitwa na mtu mmoja, akamkaribisha soda na alipokunywa tu alianza kutapika na kushikwa na kwikwi, baadaye akadondoka chini na kupoteza fahamu.

“Sisi ndugu tunajiuliza, baada ya ndugu yetu kudondoka kwa nini hakupelekwa hospitali za serikali zilizo jirani na eneo la tukio, badala yake akapelekwa Selian ambako ni mbali? Pale jirani kuna Hospitali za Tengeru, Usariver, Kilala na Ikwaranga, kwa nini asipelekwe huko karibu kama haikuwa njia ya kumchelewesha kupata huduma?
“Tulipokwenda hospitalini tulimkuta ana hali mbaya, hakuweza kuzungumza na sisi, muda mfupi baadaye akakata roho,” alisema Rose.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Sebastian Sabas alipoulizwa na mwandishi wetu kuhusu tukio hilo, alisema taarifa hiyo haijaripotiwa polisi na kuwataka ndugu wakatoe taarifa ili waanze kulifuatilia suala hilo.

Marehemu alizikwa katika Makaburi ya Makoma Old Moshi, Kilimanjaro, Januari 6, mwaka huu. Ameacha watoto wawili na mjukuu mmoja.

Leave A Reply