Aggrey Aagwa Kwa Heshima, Stars Yaibana DR Congo
KIKOSI cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kinachonolewa na Kocha Mkuu, Etienne Ndayiragije jana kimelazimisha sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya DR Congo, kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa.
Stars ilianza kufungwa dakika ya 19 kupitia kwa Fiston Mayele bao lililodumu mpaka dakika ya 45, baada ya mabeki wa Stars kufanya uzembe kuokoa hatari na kipa mkongwe Juma Kaseja kuteleza kabla ya kuokoa.
Pongezi kwa Ditram Nchimbi ambaye aliingia kipindi cha pili akitokea benchi akichukua nafasi ya Adam Adam ambaye aliweza kubadili mchezo kwa kuongeza kasi ya ushambuliaji.
Alitoa pasi dakika ya 56, iliyokutana na kichwa cha Ayoub Lyanga aliyeifungia Stars bao hilo murua.
Pia Yassin Mustapha naye alikwenda benchi nafasi yake ikichukuliwa na Edward Manyama, ambaye hakuwa na utulivu mwanzoni lakini baadaye akatulia na kuonyesha kiwango kizuri.
Kaseja naye hakumaliza dakika 90, nafasi yake ikichukuliwa na Aishi Manula, Deus Kaseke alimpisha Yusuph Mhilu. Kipindi cha pili, kiasi chake Stars ilichangamka na kufanya majaribio yaliyolenga lango tofauti na kipindi cha kwanza ambapo hawakupiga kona, shuti lililolenga lango wala lile lisilolenga lango.
Mchezo wa jana ulikuwa maalumu kwa ajili ya kumuaga mkongwe Aggrey Moris ambaye alitumia dakika 3 na nafasi yake ikichukuliwa na Karlos Potrels.Mbali na kucheza mchezo huo wa mwisho nyota huyo, alipewa milioni tano kwa ajili ya pongezi kwa huduma yake Stras na jezi iliyosainiwa na wachezaji pamoja na benchi la ufundi.
Stars sasa inajiandaa na safari yake ya kwenda Cameroon kwenye michuano ya Chan inayoanza baadaye mwezi huu.
Stori: MARCO MZUMBEDar es Salaam