The House of Favourite Newspapers

Agizo lake la usafi latekelezwa kwa kasi

0

Magufuli Rais John Magufuli.

AGIZO la Rais John Magufuli la kutaka Sikukuu ya Uhuru itakayoadhimishwa kesho, inakuwa ya kufanya usafi, limeanza kutekelezwa kwa kasi kubwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Wakati Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick leo atatoa ratiba ya shughuli za usafi ambazo zitasimamiwa na ofisi za wilaya, baadhi ya taasisi na watu binafsi, wamekuwa wanajitolea kufanya usafi katika maeneo yao ya kazi au maeneo mengine yanayowazunguka.

“Kesho (leo) nitazungumza na waandishi wa habari kuhusu jambo hilo namna Dar es Salaam tutakavyofanya usafi,” alisema Sadick jana. Juzi eneo la Kipunguni, wananchi wa maeneo hayo walijitokeza kufanya usafi wa mazingira kwa kufyeka miti na kulima nyasi pamoja na kuhakikisha wanazibua mifereji ya majitaka.

Jana pia Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo alishiriki kufanya usafi wa Jiji la Mwanza kwa kushirikiana na wafanyabiashara wa soko kuu, ambako alitumia fursa hiyo pia kuwataka walipe kodi sahihi kwa serikali.

Mjini Songea, wafanyabiashara wa samaki katika soko kuu la Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wametakiwa kufanya biashara zao za kuzingatia usafi ili kuendelea kuvutia wateja wao kununua kitoweo hicho.

Mwito huo ulitolewa jana na Mkuu wa Masoko wa Manispaa hiyo, Salum Homela alipokuwa akikabidhi vifaa vya usafi kwa wafanyabiashara wa soko hilo ili wavitumie kwa ajili ya kufanya usafi wa mazingira kuzunguka maeneo wanayofanyia shughuli zao ikiwa ni utekelezaji wa agizola Rais John Magufuli.

Homela alisema usafi kwa wafanyabiashara ni jambo la muhimu kwani itasaidia kuepusha watumiaji wa bidhaa zao uwezekano wa kupata magonjwa, yanaosababishwa na uchafu, ikiwemo ugonjwa hatari wa kipindupindu.

Alisema kuna umuhimu kwa wafanya biashara wote wakiwemo wale wa matunda, nyama, na bidhaa nyingine sokoni hapo kuzingatia usafi kwa kuwa watu wengi hasa wageni wanaotembelea manispaa hiyo, jambo la kwanza wanalohitaji kuona ni namna ya wakazi wa Songea walivyoweza kuzingatia suala la usafi wa mazingira katika maeneo muhimu yanayotoa huduma mbalimbali za kijamii.

Mjinji Sumbawanga, mkutano wa kwanza wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga uliokuwa ufanyike leo, umeahirishwa kwa kuwa wakuu wa idara wana majukumu mengine ya kusimamia usafi.

Akizungumza na gazeti hili kwa simu, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Sumbawanga, Hamid Njovu alithibitisha kwa kusema kuwa shughuli kubwa inayofanyika sasa katika manispaa hiyo ni usafi kutimiza agizo la Rais Magufuli.

Tayari msemaji wa Serikali, Assah Mwambene amewaagiza watumishi wote wa umma, kushiriki katika sherehe za Uhuru kwa kufanya usafi katika maeneo yanayowazunguka na maeneo mengine watakayopangiwa katika kupambana na kipindupindu.

Kwa upande wao, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limesema litashirikiana na wananchi kufanya usafi katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Sikukuu ya Uhuru kesho Desemba 9.

Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano wa JWTZ, Kanali Ngemela Lubinga alisema jana kuwa usafi watakaoufanya pia ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli. “Mwaka huu, Serikali imeamua kubadilisha utaratibu wake wa kawaida na shamrashamra za gwaride badala yake imeagiza kufanyika kwa usafi nchi nzima, hivyo hata sisi tutashiriki kufanya hivyo,” alisema Kanali Lubinga.

Alisema, “Usafi kwa sisi wanajeshi siyo jambo la kufundishwa, ni jadi yetu na ni tabia yetu siku zote kwa hiyo kwa kuwa kambi zetu ni safi kila siku tutaungana na wananchi wote kufanya usafi katika maeneo mbalimbali nchini.”

Kutokana na agizo hilo la Rais, taasisi na mashirika mbalimbali yamekuwa yakijitokeza kushiriki juhudi hizo za kufanya usafi wa mazingira, lengo likiwa ni utekelezaji wa agizo hilo na kuepukana na ugonjwa wa kipindupindu.

Hata hivyo, tayari Serikali ilishatoa ufafanuzi kuhusu siku ya Uhuru kwa wafanyakazi wa umma, kwamba hawatakwenda kazini, bali watabaki majumbani mwao kusherehekea kwa kushiriki kufanya usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali kama alivyoagiza Dk Magufuli.

Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imeshatoa mwongozo kwa uongozi wa mikoa hadi mitaa wa jinsi ya kushiriki usafi kesho, ambapo tayari mikoa mbalimbali ilishaanza utekelezaji wa agizo hilo kwa vitendo. Habari hii imeandikwa na Shadrack Sagati na Hellen Mlacky, Dar; Muhidin Amri, Songea, Peti Siyame, Sumbawanga na Nashon Kennedy, Mwanza.

Leave A Reply