The House of Favourite Newspapers

Aibu Yao Mameneja wa Wasanii Mateja

HIT mbili tu kwa msanii wa Bongo ni nongwa; mpigie simu sasa usikie majibu yake: “Mi siwezi kuzungumza kitu, mtafute meneja wangu.

Ukisikia hivyo unaweza kudhani kweli jamaa kaamua kuufanya muziki kuwa maisha. Siku mbili tatu baadaye utasikia huyohuyo aliyekuambia ana meneja wake kageuka kuwa teja. Anabwia unga hakuna mfano wake, akiingia kwenye shoo wapambe kibao wakiwemo hao wanaoitwa meneja. Hahihitaji elimu ya chuo kujua kazi ya meneja; kifupi ni usimamizi na uongozaji.

Tusisite kuamini mahali popote, ukiona kampuni inakufa wa kwanza kulaumiwa ni meneja; mengine hufuata. Ainisha chochote, iwe mashirika, miradi, taasisi, biashara ukiona imeyumba mzomee msimamizi na muongozaji.

Kwenye muziki nako hivyohivyo hatuwezi kuacha kuwalaumu wanaojiita mameneja wa wasanii ambao wanageuka kuwa mateja. Mwanamuziki Abubakar Katwila ‘Q Chief’ wakati akiungama makosa ya utumiaji madawa ya kulevya aliwahi kusema: “Wakati napata umaarufu nilikuwa bado mdogo halafu sikuwa na meneja wa kunisimamia.”

Enzi za kina Q Chief ni kitambo kidogo, wanamuziki walikuwa wakiishi kama kuku; wakijichunga wenyewe, lakini sasa hivi ambapo muziki umekuwa maisha lazima kuacha maneno na kuweka muziki. Kwa wasanii wa Bongo mambo mawili yanatia kinyaa. KWANZA kujiita msanii mkubwa huku ukiwa huna menejimenti ya kukusimamia na kukuongoza.

PILI; ni kwa msanii mkubwa kuwa na menejimenti halafu akajikuta amekuwa teja mikononi mwa watu ambao aligawana nao mapato ya shoo zake kama mameneja wake.

Katika dunia ya leo huwezi kuutumikia muziki mkubwa wenye hadhi kwa kuishi ya staili ya kuku tu; kufunguliwa bandani na kusepa mitaani bila kuchungwa na mtu. Matokeo yake ndiyo hayo ya kuishia kwenye madawa ya kulevya na kubaki unasinzia kama jogoo aliyekumbwa na ugonjwa wa mdondo.

Kwenye maisha kuna kanuni zake ambazo lazima zifuatwe, unapokuwa mtu wa kawaida utaishi kikawaida lakini ukijaliwa kitu tofauti lazima na maisha yawe tofauti.

Staa yeyote anayekosa msimamizi na muongozaji bora wa kazi yake lazima safari yake kimuziki na kimaisha iwe fupi. Tujifunze kilichowatoa kwenye njia Ray C, TID, Q Chief, Chid Benz, Dog Mfaume, Ferooz na wengine; ni hayo makosa mawili niliyo-sema hapo juu.

Wakati muziki umekuwa biashara kubwa bado kuna watu wanauektia! Wasanii wetu bado wanaendelea kuteketea kwa madawa ya kulevya kama nyumbu, walikoangukia akina Ray C si ajabu ukasikia Darassa naye kawa teja wa kutupwa.

Kesho keshokutwa Diamond naye anaweza kuanguka vilevile pamoja na menejimenti yake! Mara paap ukasikia Vanessa Mdee, Nay wa Mitego, na Harmonize nao wamepotea kwa njia ileile ya kugeuka mateja.

Mawili nimeshayasema; muhimu kuwa na meneja bora siyo wachumia tumbo na kingine ni kuachana na maisha ya kiholela. We umeshakuwa supastaa unawazalisha mpaka mahausigeli kwa sababu gani? Ukituambia wewe ni msanii mkubwa lazima ujiheshimu. Hivyohivyo na meneja naye, haitoshi kuitwa kiongozi wakati unayemu-ongoza anapotea mbele ya macho yako.

Risasi Vibes

Comments are closed.