AINA TANO ZA VYAKULA HATARI!

SIKU hizi afya za wananchi zipo hatarini, kutokana na ulaji wa vyakula mbalimbali ambavyo ni hatari kiafya.  

 

Leo tunaainisha aina tano za vyakula ambavyo ni hatari katika mwili wa mwanadamu licha ya kuwa vitamu kinywani, kwani vinasababisha maradhi mbalimbali. Walaji wa nyama ya nundu ya ng’ombe au nyama yenye mafuta mengi, ngozi ya kuku, chips au clips, utando wa maziwa, na bisi wapo katika hatari kubwa ya kupata magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza, ikiwamo shinikizo la damu na ugonjwa wa moyo.

 

Walaji wengi wa chipsi wapo katika hatari ya kutengeneza sumu kwenye miili yao bila kujua.

Ulaji wa chipsi ni hatari kwa afya ya binadamu, kwani husababisha maradhi mengi yasiyo ya kuambukiza hasa figo, moyo, shinikizo la damu, kisukari na saratani za aina zote.

 

Sahani moja ya chipsi kavu huwa na mafuta yanayokaribia nusu kikombe cha chai ambayo ni sawa na ujazo wa mililita 250. Si chipsi pekee ambazo ni hatari, bali vyakula vyote ambavyo hukaangwa kwa kutumbukizwa kwenye mafuta ni hatari kiafya.

Tunashauri watu waepuke ulaji wa vyakula vilivyopikwa kwa kutumbukizwa kwenye mafuta, kwani si salama kwa afya kwa sababu vyakula hivyo hunyonya kiwango kikubwa cha mafuta pindi vinapokaangwa jikoni.

 

Mwili ukipokea kiwango kingi cha mafuta (lehemu) matokeo yake ni kwamba huenda kujihifadhi kwenye mishipa ya damu hatimaye mtu hujikuta akiwa amepata shinikizo la damu na magonjwa ya moyo. Mafuta ambayo huwa na hatari kubwa zaidi ni yale yanayotokana na wanyama. Katika jamii zetu wapo watu ambao hupendelea kula nyama ya nundu inayopatikana kwenye nyama ya ng’ombe.

Hata wale wanaopenda kula ule utando wa mafuta unaotokea katika maziwa fresh yaliyochemshwa ni hatari kwa afya kwani walaji wanajiweka kwenye hatari. Nyama kama ya nundu na utando wa maziwa vina kiwango kingi cha lehemu. Ngozi ya kuku nayo ina lehemu nyingi na kwamba inapaswa kuondolewa kabla ya kuchemsha kitoweo hicho na kukiandaa kwa ajili ya kula.

 

Tunashauri kuku achunwe ngozi kabla ya kuchemshwa na kuungwa kwa ajili ya mlo, lakini pia watu waepuke kula nyama iliyonona, ni vema wale samaki na mbogamboga kwa wingi. Watu wanapaswa kupunguza ulaji wa clipsi na bisi, kwani vyakula hivyo hutengenezwa kwa chumvi nyingi ambayo baadaye huleta madhara mwilini.

 

Baadhi ya watu hupendelea kuongeza chumvi kwenye vyakula nao wanajiweka kwenye hatari ya kupata shinikizo la damu. Wapo wengine pia hupenda matumizi ya sukari nyingi matokeo yake uzito wa mwili unaongezeka, kinywa kinajaa bakteria na meno kuoza. Unywaji wa vitu vitamu ni hatari.

Hivyo basi watu waepuke kunywa vinywaji vilivyotengenezwa kwa sukari nyingi badala yake ni vema wanywe juisi za matunda ambazo hazijaongezwa sukari ya aina yoyote au maji ya madafu kwani ni salama zaidi kwa afya.

 

Wafanye mazoezi, kila siku wajitahidi kula vyakula vile vyenye asili ya nafaka, ndizi za kupika na vya asili ya mizizi kama vile mihogo na viazi, wale mbogamboga, matunda, maboga, asali na vyakula vya jamii ya kunde.

 

Nashauri ulaji wa vyakula vyenye nyuzinyuzi kwani husaidia katika uyeyushwaji wa chakula tumboni na huweza kupunguza baadhi ya saratani, magonjwa ya moyo na kisukari. Watu wapendelee kula saladi na matunda mara kwa mara, wale matunda badala ya juisi tena na maganda yake pale inapowezekana, wale ugali dona na vile vya jamii ya kunde kwani vina nyuzinyuzi kwa wingi pia wanywe maji ya kutosha.

Toa comment