The House of Favourite Newspapers

Aina ya mateso; faida na hasara zake

0

MATESO ni sehemu ya maisha ya mwanadamu, jambo hili haliwezi kupingika kwa kuwa hata mafanikio ya kimaisha hutokana na mtu au jamii kukubali kuteseka.

Pengine jambo kubwa la kujiuliza kwa kila mtu ni kwa nini anateseka? Kwa kufahamu, nimeona ni vema nilete hapa jamvini mada inayoelezea aina za mateso, hasara na faida zake ili kukufanya wewe msomaji uelimike.

MATESO YA KUJITAKIA

Mateso ya kujitakia ni yale ambayo sababu zake hutokana na mtu kutaka kushindana aidha na kanuni au taratibu za kimaisha. Kwa mfano; mtu kulala makaburini usiku, kujipa jeraha mwilini, kuua mtu anayempenda kwa lengo la kujipatia mali ni miongoni mwa mateso ambayo mtu atayapata kwa kujitakia mwenyewe.

Kama hilo halitoshi, kufanya jambo ambalo linafahamika kuwa na madhara na hatimaye kupata ugonjwa au tatizo fulani ni kujipatia mateso ya kujitakia ambayo mwisho wake huwa ni mbaya kwani wahusika wengi huishia kuwa vichaa au hujiua kutokana na kufanya vitu ambavyo lawama zake huwa juu yao wenyewe.

KUTESEKA KUTOKANA NA MAKOSA

Kama ningekuwa mhubiri pengine ningeweza kuhusisha kipengele hiki na mtu kufanya matendo ya dhambi; lakini kwa kuwa ni masuala ya kisaikolojia lazima niyapeleke kwenye mkondo huuhuu.

Kufanya mambo yoyote ya jinai na hatimaye kupata mateso ndiyo tafsiri hasa ya mateso yatokanayo na makosa. Kwa mfano, mtu anakuwa anafahamu kabisa kuwa wizi ni jambo baya, lakini anajitoa akili na kuamua kufanya kosa hilo ambalo hatimaye kumtia aidha kifungoni au kumpatia ulemavu baada ya kukatwa mikono na watu wenye hasira.

Kujipa mateso kwa kufanya dhambi kuna madhara makubwa sana mbele ya jamii kwani mtu huweza kuteseka bila kupewa msaada na wenzake au kuhurumiwa, badala yake watu hufurahia mateso yake na hivyo mhusika kujiona kama anaishi kwenye ulimwengu wa peke yake. Watu wa aina hii mara nyingi hufa ghafla tena katika mazingira ya kuhuzunisha sana.

MATESO YA KUSABABISHIWA

Mateso ya kusababishiwa ni yale matokeo mabaya ambayo mwanadamu huyapata kutokana na matendo ya binadamu mwenzake. Kwa mfano; kutiwa kilema na majambazi, kuambukizwa magonjwa kwa makusudi, kuibiwa mali, kufanyiwa ukatili wa aina yoyote, kunyang’anywa mali, yote haya ni mateso ya kusababishiwa.

Faida kubwa katika mateso ya aina hii licha ya kuwepo kwa shida kadha wa kadha, mhusika huwa na imani kubwa ambayo humfanya aishi kwa matumaini kuwa ipo siku atalipwa haki na aliyemsababishia hivyo atavuna janga la uovu wake.

Mara nyingi watu wenye mateso ya namna hii huwa na furaha kwa vile jamii huwahurumia, lakini wao nao kwa sehemu huwa na mtu ambaye humtwika lawama za mateso yao.

Kama hilo halitoshi, wanaoteseka kwa aina hii ya mateso huwa hawafi haraka kutokana na kile nilichokisema kwenye aya ya juu kuwa faraja ya binadamu wenzao huwapunguzia hisia kali za kuteseka.

Kama hilo halitoshi, uchunguzi unaonesha kuwa watu wanaoibiwa, kudhulumiwa au kunyang’anywa haki zao hufanikiwa katika maisha kwa sababu hupigania heshima zao na kutaka kuionesha jamii ushujaa wao wa kutafuta. Ukichanganya na msaada wa jamii mambo hunyooka na kuyageuza mateso yao kuwa historia.

Nawatakia uchaguzi mwema wenye AMANI.

Leave A Reply