Safari ya Kwanza ya Air Tanzania kutoka DAR – MUMBAI Yazinduliwa
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, jana, Jumatato, Julai 17, 2019, amezindua safari ya kwanza ya kimataifa ya Shirika la Ndege nchini (ATCL) ya kutoka Dar es Salaam kwenda Mumbai, India.
Kamwelwe amezindua safari hiyo, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwenye jengo jipya la safari za kimataifa ‘Terminal 3’ ambalo linatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.
Katika hafla hiyo, amewapongeza Watanzania wote ambao wamekuwa waaminifu kwa kulipa kodi kwa serikali, akisema ndiyo waliowezesha ununuzi wa ndege sita za shirika hilo na ujenzi wa jengo hilo jipya.
“Ni jitihada zenu kwenye ulipaji kodi ndizo zimewezesha kufikia mafaniko haya makubwa pamoja na mengine mengi yanayokuja, ni lazima mjipongeze,” ameeleza.
Ameongeza kuwa safari za kimataifa zitasaidia katika kukuza biashara na uwekezaji nchini, kuongeza shughuli za utalii, kuunganisha nchi na wananchi wake na mataifa mengine duniani, kukuza uchumi na kuboresha maisha ya Watanzania.
Comments are closed.