AJALI ILIYOUA WANNE…. MTOTO AIBUA SIMANZI NZITO!

NI SIMANZI juu ya simanzi! Kufuatia ajali iliyoua watu wanne katika mteremko wa Nyangoye, Bukoba mkoani hapa, mtoto wa mmoja wa marehemu ameibua simanzi nzito, Uwazi lina habari ya kusikitisha.

Ajali hiyo ilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita katika Kijiji cha Hamugembe, Bukoba na kuua watu hao wanne ambao ni Nice Masanja aliyekuwa dereva wa gari aina ya Hiace (daladala) na utingo wake, Peter Ifunya.

Wengine ni Prudence Themistocles aliyekuwa mwendesha pikipiki na Dickson Bakuza aliyekuwa dereva wa Canter ambao wote walikufa eneo la tukio.

 

MTOTO AIBUA SIMANZI

Katika tukio hilo, kilichowaumiza wengi na kuongeza uzito wa simanzi ni kifo cha dereva wa daladala, Nice ambaye ameacha watoto watatu huku mmoja, Ivan Nice akiwatoa watu machozi.

Wakati baba yake akifariki dunia kwenye ajali hiyo, ilikuwa ni siku chache tangu Ivan alipopata ajali ya kuungua kwa maji ya moto.

Ivan aliungua sehemu kubwa ya mwili wake alipokuwa akicheza na mtoto wa jirani yao hivyo wakati baba yake akiaga dunia, yeye alikuwa akiuguzwa nyumbani.

Machozi zaidi yalitawala kwenye familia hiyo kwani dereva huyo (Nice) ndiye aliyekuwa tegemeo kwa ajili ya kumuuguza Ivan.

 

Kwa mujibu wa mke wa Nice, Adelina Marchol (34), kabla ya umauti kumkuta, mumewe aliondoka nyumbani asubuhi kuelekea kazini mara baada ya kupigiwa simu na tajiri wake (mmiliki wa daladala) akimtaka aende na leseni yake.

Alisema baada ya kupakia abiria na kuondoka kuelekea Mutukula, wakiwa njiani wakirejea, walipofika Rwamisheneye ambapo ndipo makazi yao yalipo, alimpigia simu akimfahamisha kuwa amerejea salama na mizigo aliyokuja nayo angeipeleka nyumbani baada ya kushusha abiria. Mama huyo alisema kuwa, baada ya hapo, simu aliyoipata nyingine ilikuwa ya dereva ambaye ni rafiki wa mumewe akimtaarifu habari za ajali na msiba.

 

AJALI ILIKUWAJE?

Ilikuwa usiku wa Februari 8, mwaka huu ambapo vilio na simanzi vilitawala katika kijiji hicho cha Hamugembe, Nyangoye Manispaa ya Bukoba, eneo maarufu kwa matukio ya ajali zilizogharimu maisha ya watu wengi.

Ilikuwa majira ya saa tatu usiku ambapo kilisikika kishindo kikubwa cha ajali iliyohusisha magari mawili yaliyogongana uso kwa uso.

Magari hayo ni lori dogo aina ya Canter, mali ya Jibril na gari ndogo la abiria almaarufu daladala linalofanya safari zake kutoka Bukoba kwenda Mutukula.

 

Kwa mujibu wa shuhuda wa ajali hiyo, Abdul Itembwe, tukio hilo lilitokea katikati ya mteremko wa Hamugembe ambapo daladala hilo lilikuwa likipanda na Canter ikiteremka.

“Gari aina ya Canter lilipata hitilafu upande wa breki na kusababisha kugonga daladala kisha kuserereka nalo hadi kando ya barabara, yapata mita 150 kutoka katikati ya barabara.

“Hali hiyo ilimkumba mwendesha pikipiki aliyefahamika kwa jina la Prudence, mkazi wa Nyakanyasi ambaye alijikuta akizolewa na magari hayo kisha kupoteza maisha eneo la tukio .

 

“Kufuatia magari hayo kugongana, mara baada ya kuwa tayari yamesimama, zilianza kuibuka cheche ndogondogo upande wa daladala wakati jitihada za uokoaji zikiendelea kujaribu kuwanasua watu kwenye tukio hilo,” alisimulia shuhuda huyo.

Aliongeza kuwa, ghafla moto mkubwa ulilipuka na kuanza kuunguza gari hilo huku ndani kukiwa na watu watatu ambao walionekana kupoteza fahamu kama siyo kufariki dunia.

Wakati hayo yakiendelea, upande wa lori ambalo lilikuwa na abiria wawili na dereva, abiria hao walifanikiwa kunusurika na kutoka kupitia dirisha la mlango wa abiria kabla ya kushika moto.

 

Wakati jitihada za uokoaji zikiendelea, ilidaiwa kwamba dereva wa lori, Dickson (25) alijitahidi kujinasua, lakini haikuwa rahisi huku akipiga kelele kuomba msaaada.

Licha ya wasamaria wema kufika eneo hilo na kuanza kumvuta dereva huyo wa lori, lakini alikwama hadi mauti yanamkuta huku akisema; “Asanteni kwa msaada wenu mimi ninakufa…”

 

Hadi Jeshi la Polisi na lile la Uokoaji (Zimamoto) wanafika eneo la tukio, tayari moto ulishawazidi wananchi ambao awali walionesha juhudi za kuuzima kwa maji na mchanga.

Jeshi la Polisi mkoani Kagera lilithibitisha vifo vya marehemu hao.

Stori: Abdullatif Yunus, Kagera.


Loading...

Toa comment