Ajali Moro: Mwingine Afariki, Utambuzi Tatizo kwa Mahututi – Video

MAJERUHI mwingine mmoja wa ajali ya lori la mafuta iliyotokea Morogoro aliyekuwa akipata matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es salaam amefariki dunia usiku wa kuamkia leo na kufanya idadi ya watu waliofariki kutokana na ajali ya moto iliyotokea Jumamosi, Agosti 10, 2019, kufikia 76.

 

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne, Agosti 13, 2019, Msemaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Eligaisha, amesema  majeruhi wa ajali hiyo wanaendelea vizuri.

 

“Hali za majeruhi zinatia matumaini, tulipokea wagonjwa 46 hapa Muhimbili kutokea Morogoro, hadi sasa idadi yao wamefikia 38 ambao 25 wanajitambua na waliobaki 13 wapo ICU hawajitambui, waliofariki ni wagonjwa wanane,” amesema.

 

“Wengi wao wametambuliwa na ndugu zao, lakini wapo ambao hawawezi kuzungumza na wapo ICU, hao imekuwa vigumu kidogo kuwatambua ndugu, kumekuwa na mgongano. Anakuja mtu mmoja anasema huyu ni ndugu yangu, anakuja mwingine naye anasema huyu ni ndugu yangu, mkiwauliza umemtambuaje, anasema alikuwa amenyoa kiduku.

 

“Ukiangalia wengi wao walikuwa vijana na walikuwa wamenyoa viduku, kwa hiyo si rahisi kumtambua mtu kwa kiduku. Mwingine anasema ana mguu mkubwa, wengi wao wameungua asilimia 80 hadi 90, hivyo wamevimba,” amesema Eligaesha.

 

Aidha, amesema  Hospitali ya Muhimbili inashirikiana na ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili kuchukua vipimo kwa watu hao wanaodai kuwa ni ndugu wa majeruhi kwa ajili ya utambuzi.


Loading...

Toa comment