The House of Favourite Newspapers

AJALI YA MV NYERERE… ALIYEACHIWA WATOTO 6 AIBUA SIMANZI

MWANZA: AMA kweli kila aliaye hushika kichwa chake mwenyewe; ajali mbaya ya Kivuko cha Mv Nyerere iliyoua mamia ya watu iliyotokea hivi karibuni kisiwani Ukara, Ukerewe mkoani Mwanza imeacha simanzi tofautitofauti kwa kila Mtanzania aliyeguswa na ajali hiyo.  

 

Ni wazi kwamba wapo waliohuzunika kwa kupoteza dada, kaka, shemeji waume, wake, ndugu na jamaa zao; na kuwaombolezea kwa namna tofauti; lakini kwa Samweli Malima mkazi wa Urasa aliyeachiwa watoto sita na mkewe aitwaye Zawadi Januari aliyekufa maji katika ajali hiyo, anaona dunia yote imeinama.

Malima anaeleza kuwa siku ya ajali hiyo hakuona dalili zozote za yeye kutoonana milele na mkewe na kwamba waliagana kwa upendo kwa matumaini kuwa wataonana jioni mara baada ya mke kurejea kutoka gulioni Ukerewe. “Kila Alhamisi huwa kuna gulio (minada ya kuuza na kununua vitu mbalimbali), mke wangu alikwenda gulioni akaniachia hawa watoto wetu sita niwaangalie yeye apeleke bidhaa akauze.

 

“Tumeshinda vizuri na watoto wangu. Jioni, ikaanza minong’ono kuwa kivuko kimezama, nilishtuka sana, watu tukaanza kukusanyika, kwa kuwa si mbali sana na sehemu ya kuweka nanga, wengi tulikiona kile kivuko lakini hakuna aliyekuwa na uwezo wa kwenda kusaidia kitu chochote.

 

“Hisia za mke wangu kufa maji ziliponijia nilipingana nazo maana niliona kama nataka kuzimia, nikawa najipa moyo kwamba ataokolewa akiwa hai,” alisema Malima huku akifuta machozi. Hata hivyo matumaini yake hayakuwa hivyo kwani mkewe alipoteza maisha katika ajali hiyo na kuacha watoto sita ambao bado wangali wadogo.

Simulizi ya kusikitisha aliyoitoa Malima ni pale alipoeleza kuwa tangu imetokea ajali hiyo, watoto wake hasa wenye miaka 3, 1 wamekuwa wakimpa wakati mgumu kwa kumuuliza: “Mama yuko wapi? “Kitu kigumu kwangu ni hawa watoto, wananiumiza sana wakiniuliza, hata nikiwaambia mama yao kafariki hawanielewi wanachodai ni zawadi aliyoahidi mama yao kuwaletea akitoka mnadani.

 

“Kweli wanasema hujafa hujaumbika, leo wanangu wamebaki yatima…” Malima analia kwa uchungu huku akitazama angani pengine ni ishara ya kushukuru Mungu au vinginevyo. Kwa upande wa jirani zake Malima nao walikuwa na huzuni isiyoelezeka kutokana na eneo hilo kuwa na misiba mingi ambapo wakazi wa eneo hilo la Ukara wengi wanafahamiana na kwamba kila msiba uliwagusa wakazi wa eneo hilo.

 

Kivuko cha MV Nyerere kilizama Alhamisi, Septemba 20 mwaka huu kilometa 50 kutoka Kisiwa cha Ukara ambapo watu zaidi ya 200 waliripotiwa kupoteza maisha huku watato wakiwa ni wa familia moja. Kufuatia ajali hiyo mbaya, Rais John Magufuli alitangaza siku 4 za maombolezo ambapo bendera ilipepea nusu mlingoni huku akiagiza uchunguzi wa haraka ufanywe kujua chanzo cha ajali hiyo.

STORI: MWANDISHI WETU, UWAZI

MAJONZI! Mume, watoto walipoonyeshwa kaburi la mama yao!

Comments are closed.