Ajibu amtumia ujumbe kocha Stars

IKIWA zimebaki siku tisa kabla Taifa Stars haijacheza na Uganda kwenye mchezo wa kutafuta tiketi ya kucheza Kombe la Mataifa Afrika kiungo wa Yanga, Ibrahim Ajibu, amemtumia kocha wa timu hiyo ujumbe kwa vitendo.

 

Mashabiki wa soka wamekuwa wakinung’unika chinichini kutokana na kocha wa Stars, Emmanuel Amunike kutomwita kiungo huyo kwenye timu ya taifa pamoja na kwamba amekuwa akifanya mambo makubwa uwanjani.

 

Ajibu wikiendi iliyopita alionyesha kuwa bado yupo kwenye chati baada ya kupiga pasi yake ya 15 ya bao kwa msimu huu baada ya kuiongoza timu yake kushinda kwa mabao 2-1 dhidi ya KMC. Huu ni ujumbe tosha kwa kocha huyo kuwa anakosea kutomjumuisha mchezaji huyo kwenye timu hiyo.

 

Mbali na huyo, pia Amunike ameshindwa kumuita kinara wa ufungaji kwenye ligi kwa sasa Salim Aiyee wa Mwadui ambaye amefunga mabao 15. Aiyee naye alimtumia ujumbe kocha huyo kwa kufunga bao moja wikiendi iliyopita baada ya timu yake kuifunga Mbeya City mabao 3-1.

Toa comment