Ajibu Awatikisa Wazungu

KIUNGO wa Yanga Ibrahim Ajibu ameweka rekodi ya kipekee baada ya hadi sasa kuwa kinara wa pasi za mwisho (asisti) kwenye ligi kadhaa kubwa duniani.

 

Ajibu anaongoza kwa kupiga pasi za mwisho kwenye Ligi Kuu Bara kwa sasa akiwa ameshapiga pasi 12, akiwa zaidi hata ya Lionel Messi mwenye pasi kumi.

 

Ajibu ambaye pia msimu huu hakucheza michezo kadhaa ya mwanzoni ameonekana kuwa kiungo matata zaidi haswa kwa pasi zake za mbali.

 

Kwenye Ligi Kuu England, kinara wa pasi ni Ryan Fraser wa timu Bournemouth ambaye ameshapiga pasi saba hadi sasa, akiwa amezidiwa na Ajibu kwa pasi tano.

Katika Ligi Kuu ya Ufaransa kinara wa pasi ni Memphis Depay anayeichezea Olympic Lyon ambaye ameshapiga pasi sita nusu ya zile alizopiga Ajibu.

 

Sehemu pekee ambayo Ajibu amezidiwa ni kwenye Ligi Kuu ya Ujerumani ambapo Thomas Muller ana pasi 14 akiwa amemzidi Ajibu mbili na Joshua Kimmich anayeshika nafasi ya pili ana pasi 13 akiwa amemzidi kwa pasi moja.

 

Kwenye chati ya ufungaji, Ajibu amefanikiwa kufunga mabao matano, hivyo amehusika kwenye mabao 17 ya timu yake hadi sasa kati ya 33 ambayo timu yake imefunga.

Mwandishi Wetu,

Toa comment