IMEFAHAMIKA kuwa mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu, huenda akaukosa mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya St Louis ya Shelisheli kutokana na majeraha ya goti ambalo pia linamsumbua Mrundi, Amissi Tambwe.
Mshambuliaji huyo, tayari amekosa michezo miwili; mmoja wa Kombe la FA timu hiyo ilipocheza dhidi ya Ihefu FC ya Mbeya na Ligi Kuu Bara waliocheza juzi Jumamosi dhidi ya Lipuli FC ya Iringa ambayo yote walishinda.
Awali, kulikuwa na usiri mkubwa wa tatizo la mshambuliaji huyo la kutocheza michezo hiyo miwili ya mfululizo, licha ya tetesi kuwepo ana majeraha.
Ajibu kupitia ukurasa wake wa Instagram, jana alitupia picha akiwa maabara hospitalini akifanyiwa vipimo kwenye goti la kushoto.
Picha hiyo iliendana na maneno yake mazuri kwa ajili ya kuwafahamisha mashabiki wa timu hiyo waliokuwa wakihoji sababu ya kutocheza michezo hiyo miwili.
Aliandika hivi akiambatanisha maneno yake na picha: “Habari zenu wapendwa, najua mlitamani sana niwepo kwenye ‘game’ yetu ya jana (juzi) ila hali halisi ndiyo hii.”
Kwa mujibu wa daktari mkuu wa timu hiyo, Edward Bavu, mshambuliaji huyo alipata majeraha hayo ya goti kwenye mechi ya ligi kuu dhidi ya Azam iliyomalizika kwa Yanga kushinda mabao 2-1.
“Ajibu tulimbakisha Dar kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya goti lake kabla ya kuanza matibabu, ni baada ya kuumia mechi na Azam.
“Hatima yake ya kucheza mechi ya kimataifa tutakayocheza Jumapili itajulikana baada ya kupata vipimo vya jeraha lake, hivyo tunaomba muda kidogo na taarifa zake zitatolewa,” alisema Bavu.
Wilbert Moland, Dar es Salaam
Comments are closed.