The House of Favourite Newspapers

Ajibu: Bado naipenda Yanga SC

Ibrahim Ajibu

STAA wa Simba, Ibrahim Ajibu Migomba, amefunguka kuwa haitakuwa ajabu kwake kurudi Yanga kwa kuwa bado anaipenda klabu hiyo.

 

Ajibu ambaye kwa sasa yupo na Simba Afrika Kusini kwenye kambi, amesaini mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia Simba akitokea Yanga aliyokuwa nayo kwa msimu uliopita.

 

Usajili wa Ajibu Simba ulikuwa gumzo kutokana na staa huyo kuwa miongoni mwa wachezaji wa Yanga ambao waliondoka na kutua Msimbazi. Wachezaji wengine ni Beno Kakolanya na Gadiel Michael.

 

Kiungo huyo ambaye msimu uliopita aliongoza kwa pasi za mabao, ameliambia Championi Ijumaa, kuwa mapenzi yake kwa Yanga bado yapo makubwa na anaweza kurejea ndani ya kikosi hicho kwa misimu ijayo.

 

“Bado nawapenda sana Yanga, kwa muda wote ambao nilikaa nao, lakini hata kama mtu unampenda huwezi kukaa naye miaka yote. “Kwa muda wote huo hawajanikosea, nimeondoka kwa wema tena sina matatizo na mtu yeyote yule. “Nikihitaji kurudi Yanga baada ya kutoka hapa Simba basi nitarudi tu,” alisema Ajibu.

Comments are closed.