The House of Favourite Newspapers

Ajibu kawatetee wale waliokuwa wanakutetea

BAADA ya maneno mengi, hatimaye kiungo wa Yanga, Ibrahim Ajibu juzi aliitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars.

 

Ajibu aliitwa kwenye timu hii ambayo inajiandaa na michuano ya Kombe la Mataifa Afrika ambayo inaanza mwezi ujao nchini Misri.

 

Kwa maelezo ya kocha wa timu hiyo, Emanuel Amunike, ameita timu yenye wachezaji wengi kwa kuwa watagawanywa kwenye vikosi viwili kile kitakachocheza CHAN na kila cha Afcon.

 

Tangu alipotua hapa nchini, Amunike alikuwa akilaumiwa na mashabiki wa soka kwa kitendo chake cha kutomuita Ajibu. Hili lilikuwa moja ya jambo ambalo lilishusha thamani ya kocha huyo raia wa Nigeria.

 

Lakini kitendo cha kumuita sasa kwenye timu hiyo kinaonyesha kuwa amepunguza presha kwake na labda amesikiliza yale yaliyokuwa yanazungumzwa na wadau. Ajibu anaitwa akiwa ni mchezaji wa pekee kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, amepiga pasi 16 za mabao akiwa ndiye kinara na wanaomfuata wapo nyuma sana.

 

Hii inaonyesha kuwa sasa Amunike ameuona uwezo wa kiungo huyo, lakini pamoja na hapo bado kuna maswali mengi sana, mojawapo ni Ajibu sasa kuhakikisha kuwa anarudisha fadhila za wale mashabiki ambao kila kukicha walikuwa wanataka aitwe kwenye timu hiyo.

 

Mashabiki wengi waliamini kuwa Ajibu anaweza kuisaidia Stars ndiyo maana wakawa wanapiga kelele za kutaka aitwe, sasa ni muda wake wa kumuonyesha Amunike kuwa alichelewa kumuita. Aonyeshe uwezo wa juu na nidhamu nzuri kwenye timu hiyo, badala ya kubaki na ya kuonyesha utovu wa nidhamu.

 

Sasa Ajibu anatakiwa kuhakikisha kuwa anakuwa wa kwanza kwenye kila kitu, kama ni kuwahi mazoezini na juhudi uwanjani, basi afanye hivyo. Ajibu amekuwa akilaumiwa kwa kuwa mvivu mazoezini, amekuwa akisemwa sana kuwa nidhamu yake kwa sasa imeshuka basi abadilike kwenye hili na kuwa mchezaji sahihi mwenye kiwango kile ambacho mashabiki waliokuwa wanapiga kelele kuwa aitwe.

 

Lakini jambo lingine zuri ni kuitwa kwa Kelvin
John maarufu kama Mbappe, anaweza asicheze mchezo hata mmoja kwenye timu hiyo kwa sasa.

 

Lakini hii ni heshima kwake kutokana na kile ambacho amekionyesha kwenye michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa vijana iliyomalizika hivi karibuni. Kijana huyo alionyesha kiwango cha juu sana kwenye michuano ile na kuitwa kwake sasa ni picha halisi kuwa ukionyesha juhudi unaweza kuheshimiwa.

 

Huyu anawafanya wale vijana wengine ambao walikuwa kwenye michuano hiyo kuendelea kupambana ili wafikie hapa alipofika staa huyo.

 

Kuitwa kwenye timu hii tu hakutoshi, Mbappe anatakiwa sasa kuhakikisha kuwa anaonyesha juhudi akiwa kijana mdogo ili asitoke kwenye timu hiyo tena. Dogo huyo anaweza kuweka rekodi kwenye timu hiyo kama ataonyesha juhudi na kuacha kuvimba kichwa.

 

Kuitwa kwenye timu ya Taifa ukiwa na umri kama huu wakati mwingine ni mtihani mzito kwa kuwa kuna mambo mengi unatakiwa kuyapitia kama hujafikia kwenye kiwango cha juu.

Comments are closed.