The House of Favourite Newspapers

Ajibu, Ngassa Wapewa Kazi Maalum ya ‘Kumpikia’ Makambo

Heritier Makambo.

VIUNGO washambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu na Mrisho Ngassa, jana walipewa kazi maalum ya kuhakikisha wanapiga krosi safi kwa washambuliaji wao katika kujiandaa na mchezo dhidi ya Simba.

 

Timu hizo, zinatarajiwa kuvaana kesho Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam unaotarajiwa kujaa upinzani mkubwa kutokana na umuhimu wa mchezo huo.

 

Viungo hao, walipewa kazi maalumu hiyo na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mkongoman, Mwinyi Zahera wakati timu hiyo ikifanya maandalizi yake ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba.

Kocha huyo katika mazoezi yake aliwatengea mipira Ajibu na Ngassa na kuwataka wawapigie washambuliaji wake Amissi Tambwe, Heritier Makambo pamoja na mabeki wake Andrew Vicent ‘Dante’ na Abdallah Shaibu ‘Ninja’ kuicheza mipira hiyo.

Wakati akiendelea na program hiyo, kocha huyo alikuwa akiwataka Ajibu na Ngassa kupiga mipira mizuri ya krosi itakayowafikia kichwani nyota hao kabla ya kufunga.

 

Kocha huyo, pia aliwataka viungo hao kupiga mipira ya krosi kwa washambuliaji na mabeki hao aliowandaa kwa ajili ya kufunga mabao. Mazoezi hayo, yakiendelea kuna wakati alionekana akisimamisha mpira na kuwataka kupiga kwa ufanisi huku akitoa mfano halisi wa kuupiga mpira yeye mwenyewe pale anapoona wanakosea.

Katika mazoezi hayo, Tambwe, Makambo na Ninja walionekana kucheza vizuri kwa kufuata maelekezo hayo ya kocha aliyokuwa anayatoa kwenye Uwanja wa Chuo cha Biblia hapa Bigwa, Morogoro. Baada ya mazoezi hayo, Zahera alisema: “Hiyo ni moja ya mbinu yangu nitakayoingia nayo katika mechi hiyo, ninataka mabao yatokee sehemu zote kwa maana ya katikati na pembeni kwa kutumia mipira ya krosi.

 

“Hivyo, ninafurahia kuona vijana wangu wakifuata maelekezo yangu vizuri kwa kutumia vema mipira ya krosi na kona walizokuwa wanazipiga na kikubwa ninataka kuona hii ikifanyika katika mechi,” alisema Zahera.

Comments are closed.