The House of Favourite Newspapers

AKIMBIWA KISA, UGONJWA WA KIFUA KIKUU

 

MKAZI wa Mbezi Makabe, jijini Dar es Salaam, Upendo William, amelalamikia kile alichodai kuwa kutelekezwa na mume wake wa ndoa iliyodumu kwa takriban miaka 20, baada ya kuugua ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) kwa zaidi ya mara mbili.

Akizungumza na UWAZI mwishoni mwa wiki iliyopita, Upendo ambaye pia ni mzaliwa wa mjini Dodoma, alisema yeye na mume wake walifanikiwa kufunga ndoa mnamo mwaka 1999, na kubahatika kupata watoto wawili. Akielezea tatizo hilo alikuwa na haya ya kusema:

“Mimi ni mzaliwa wa Dodoma, nimefunga ndoa na mume wangu tangu mwaka 1999, na tukajaliwa kupata watoto watatu,. Mwezi wa nne mwaka janandio alinitelekeza, akaniacha nikiwa naumwa ugonjwa wa Kifua Kikuu, nilioupata mwaka 2015.

“Baada ya kufuatilia niligundua kuwa ana mwanamke mwingine nje ya ndoa niliwafuma, niliumia sana kwa wakati ule, mume wangu alikuwa akinisema vibaya na kusema nimeenda kutafuta nini pale, mwisho yule mwanamke wake alikuja na kuanza kunipiga, na kuchukua vitu vyangu vyote.

“Hakuishia hapo, baada ya kuondoka ile sehemu nilirudi nyumbani kwangu huku nikiwa na maumivu makali lakini baada ya muda kupita yule dada (mwanamke mwenzake) alikuja nyumbani kwangu kufanya fujo mpaka akanivunjia mlango, baada ya hapo nilikwenda kushtaki polisi lakini kesi ikaishia hewani,”alidai Upendo huku akitokwa machozi.

Miaka miwili ilivyopita mwanamama huyo anasema, alikunywa dawa za TB kwa mara ya kwanza akapona, baada ya hapo mume wake alimfuata na akamtaka wazae tena mtoto wa tatu.

“Kwa miaka miwili nimeteseka, nilikunywa dawa za TB mara ya kwanza nikapona, ila baada ya hapo mume wangu alirudi akaniomba msamaha na kuniomba tuzae tena mtoto watatu, kwa kuwa bado nilikuwa nampenda nilimkubalia, ila baada ya kukubali kubeba ujauzito wa tatu nilipata tena ugonjwa huo wa TB kwa mara ya pili, na nikaanza kutumia dozi nikiwa na ujauzito.

“Tulifanikiwa kupata mtoto watatu, ambapo akarudi tukakaa kidogo akaondoka tena, ndipo kuanzia hapo akaja akanitelekeza yaani hanithamini wala hanijali,”alidai Upendo. Alipoulizwa kuhusu maendeleo ya watoto wake hao watatu, na mume wake yupo wapi alisema, mume wake alikuja kuwachukua watoto wawili ambapo mmoja yupo kwa shangazi yake Buguruni Malapa na mmoja hafahamu alipo mpaka sasa.

“Mume wangu alikuja akawachukuwa watoto wangu wawili, ambapo mmoja wa miaka minne alimpeleka kwa shangazi yake ambaye anaishi Buguruni Malapa, ila huyo mtoto wangu mwingine sifahamu alipo mpaka sasa. Mume wangu pia sijui alipo kwa sababu hata mawasiliano yake sina.

“Nawaomba Watanzania wanisaidie kama wanavyoniona, nimedhoofu kwa sababu sipati lishe bora, nilienda kupima vipimo vyote niko salama na hata ile TB pia madaktari waliniambia nimeshapona.

“Mwili wangu unazidi kuporomoka kwa kuwa nina mawazo sana, nawawaza sana wanangu, hasa huyu ambaye sijui alipo mpaka sasa, na hata huyu wa miaka minne nikitaka kwenda kumuona wifi yangu ananifukuza, na kunifungia mlango hataki hata kuniona.

“Hapa nilipo nimebaki mimi na mtoto wangu mmoja ambaye yupo darasa la saba na anakaribia kufanya mitihani ila chakula kwetu imekuwa shida sana, na hapa tunapoishi kodi ya nyumba imeisha na mwenye nyumba anahitaji hela yake,” alisema Upendo huku akifuta machozi kwa khanga.

Gazeti hili lilibahatika kuzungumza na majirani zake, ambapo mmoja aliyejitam-bulisha kwa jina la Mariam Seif, alikiri kumfahamu Upendo.

“Ni kweli amekimbiwa na mume wake baada ya kuugua huo ugonjwa, binafsi huwa najitahidi sana kumpatia kile ambacho mimi pia najaliwa, lakini kama mnavyoona hali yake kwa sasa ni mbaya, ndipo nilipowashauri wenzangu tuwatafute waandishi wa habari ili waweze kumsaidia, ila kiukweli huyu dada anateseka sana maana chakula chenyewe mpaka aombe kila siku,” alisema Mariam.

Kwa yeyote aliyeguswa na habari hii anaweza kumsaidia Upendo kwa kutumia namba

0675 800 925.

Stori: Memorise Richard na Neema Adrian, Uwazi

Comments are closed.