The House of Favourite Newspapers

Akutwa Ameuawa Ndani, Mwili Umeharibika, Mjumbe Asimulia – Video

0

MWILI wa mke wa Dickson Ponela, Prisca John Sambu (35) umekutwa umeharibika chumbani ambapo mashuhuda waliouona kwa mara ya kwanza walidai kuwa mwanamke huyo ameuawa.

 

Kilichowasukuma baadhi ya watu kuamini kuwa Prisca ameuawa na asiyejulikana ni mazingira ya tukio hilo la kusikitisha lililotokea Jumatatu iliyopita maeneo ya Kipunguni A, jijini Dar kwenye nyumba aliyokuwa akiishi mwanamke huyo.

 

Chanzo kilisema kuwa mwili wa mwanamke huyo ambaye ni mama wa watoto wawili, ulikutwa kitandani ukiwa umeharibika baada ya kukaa kwa zaidi ya siku mbili bila kugundulika.

 

“Vitu ikiwemo TV, vilikutwa vimesambaa chumbani kuonesha kuwa kulikuwa na vurugu kabla ya kifo cha mwanamke huyo,” shuhuda wa tukio hilo alidai huku akiomba kufichwa jina lake.

Hata hivyo duru za kipolisi hazijatoa tamko lolote kuhusiana na kuuawa au ukweli mwingine juu ya kifo hicho.

 

Hata hivyo, madai mazito kutoka kwa baadhi ya mashuhuda yamesema ‘skana’ za macho yao zilionesha kuwa mwili wa Prisca ulikuwa na michubuko na hivyo kuomba uchunguzi wa polisi ufanyike kwa kina.

“Ni jirani yangu, rafiki yangu pia naamini kwa asilimia nyingi tu kuwa marehemu ameuawa,” alisema rafiki wa marehemu ambaye hakupenda kutajwa jina gazetini.

 

Ni vipi madai hayo yaaminike kimebaki kuwa kitendawili kwani hata watoa maelezo wamekuwa na maneno matupu yasiyoambatana na ushahidi wowote.

 

MAREHEMU ALIKUWA AMETENGANA NA MUMEWE

Habari kutoka eneo la tukio zinaonesha kuwa marehemu Prisca alikuwa ametengana na mumewe Ponela mwaka mmoja uliopita na kwamba alikuwa akiishi peke yake mahali ambapo umauti ulimfika.

Akizungumza kwa masikitiko makubwa baba wa marehemu Prisca aitwaye John Sambu alisema:

“Kifo cha mwanangu kimeniuma sana, ni kweli binadamu huwa tunakufa lakini kifo hiki kimeniuma zaidi.”

 

Alipoulizwa na wanahabari wetu kama alikuwa akihisi utata wowote kufuatia kifo cha mtoto wake, mzee Sambu alisema:

“Ninachojua ni kwamba mwanangu aliachika na huyu mumewe kama mwaka mmoja na miezi kadhaa, sasa nilipokuwa nikimtazama ni kama alikuwa na msongo wa mawazo.

 

“Alikuwa anakunywa pombe sana na wakati mwingine hakuonesha kuwa na furaha.

“Basi ndiyo hivyo, huwenda pia yapo mengine yaliyochangia kifo chake maana hata polisi wameniambia jambo na kuniomba tuzike kwanza tuwaache wao waendelee na uchunguzi.

 

POLISI WACHUKUA SIMU NA VIELELEZO VINGINE

Kufuatia tukio hilo, polisi baada ya kufika eneo la tukio waliuchukua mwili wa marehemu Prisca na kuupeleka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kuufanyia uchunguzi huku wakichukua pia simu ya marehemu pamoja na vielelezo vingine.

 

Habari za kipolisi ziliwaambia waandishi wetu kuwa hakuna kitu kitakachoshindwa kubainika katika kifo hicho na kwamba taarifa zaidi zitatolewa baada ya upelelezi kukamilika.

“Mlitaka kuambiwa nini? Uchunguzi unaendelea, sasa tukiwaambia kila kitu tutakuwa tunachunguza nini tena,” Afisa mmoja wa polisi alisema na kuomba asitajwe jina kwa sababu yeye si msemaji wa jeshi hilo.

 

MJUMBE WA MTAA AFUNGUKA

Naye Mjumbe wa Mtaa wa Kipunguni A, alipokuwa akiishi Prisca, aitwaye Khalid Sabuni alipotafutwa kuhusiana na tukio hilo alikiri kutokea.

“Nilipigiwa simu na baba wa marehemu na mimi kama mjumbe nilikwenda eneo la tukio, nilipofika nikakuta mwili ukiwa kitandani. Nikawapigia simu polisi na hao ndiyo wenye majibu ya kifo hicho.”

 

WAANDISHI WASHUHUDIA MAZIKO

Baada ya kutoka eneo la tukio, Jumatano wiki hii waandishi wetu walifanikiwa kuhudhuria maziko ya Prisca yaliyofanyika eneo la Wazo, Tegeta nyumbani kwa mume wake.

 

Habari zinasema kuwa sababu za Prisca kuzikwa nyumbani kwa mumewe licha ya kuwepo kwa taarifa kuwa walikuwa wameachana ni katika kudumisha mila za Kikurya ambalo huamini kuwa mwanamke aliyeolewa lazima azikwe na mumewe bila kujali wameachana au la!

 

LULU MAJIZO WAIBUKA MSIBANI

Katika kuonesha hali ya kujali, staa wa filamu za Kibongo Elizabeth Michael ‘Lulu’ na mchumba wake Francis Siza ‘Majizo’ waliibuka msibani hapo.

Waandishi wetu walimshuhudia Lulu na mchumba wake wakiwa sehemu ya watu walioonekana kuwa na ukaribu na msiba wa Prisca.

 

RPC ILALA ATAFUTWA

Katika kujua kinachoendelea upande wa polisi, wanahabari wetu walimpigia simu Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Kamishna Msaidizi (ACP) Zuberi Chembera ambapo simu yake ilipokelewa na afande aliyejitambulisha kwa jina la PC Mussa ambaye alisema muda huo bosi wake alikuwa na majukumu ya kikazi na kwamba asingeweza kuzungumza na wanahabari.

STORI: NEEMA ADRIAN NA RICHARD BUKOS

Leave A Reply