The House of Favourite Newspapers

Akutwa na meno ya bandia kwenye koo

MGONJWA mmoja nchini Uingereza amejikuta katika maumivu makali baada ya meno yake ya bandia kunasa kooni kwa wiki moja. Mgonjwa huyo mwenye miaka 72 alikuwa akilalamika kupata maumivu makali wakati wa kumeza vitu na kukohoa damu katika kipindi chote hicho. Bwana huyo, alimeza meno hayo wakati akifanyiwa upasuaji wa tumbo.

Undani wa tukio hilo umechapishwa kwenye jarida la kisayansi la BMJ ambapo watunzi wake wamewataka madaktari kuhakikisha wagonjwa wao wanaondoa meno ya bandia kabla ya upasuaji. Siku sita tu baada ya upasuaji huo uliofanyika mwaka 2018, bwana huyo alienda kwa daktari na kulalamika kuwa nanashindwa kumeza vyakula vizito.

Madaktari awali waliamini kuwa hiyo ni athari ya kuwekewa mpira kwenye kinywa wakati wa upasuaji, na kumpatia dawa za kukabiliana na maumivu na maambukizi ya koo. Lakini baada ya bwana huyo kurudi tena baada ya siku mbili akiwa na malalamiko zaidi, madaktari ikabidi wamfanyie uchunguzi zaidi wa koo. Vipimo vya miale ya X-Ray vikaonYesha kuwa kuna meno ya bandia matatu na chuma chake cha kuyashikilia.

Baada ya hapo, mzee huyo akawaambia madaktari kuwa alipoteza meno yake ya bandia katika kipindi ambacho alilazwa hospitalini kwa upasuaji wa tumbo. Ikalazimika afanyiwe upasuaji wa haraka wa koo, lakini akarudi hospitali mara nne zaidi ili kuongezewa damu. Watafiti wameeleza katika ripoti yao kuwa kuna zaidi ya mkasa mmoja wa watu kumeza meno ya bandia wakati wakipigwa dawa za usingizi. Uwepo wa meno bandia ama kifaa chochote cha bandia kinywani, unatakiwa uripotiwe kabla na baada ya upasuaji, wamesisitiza kwenye ripoti ya jarida hilo.

Hazel Stuart, ambaye ni mkurugenzi wa matibabu katika hospitali ya Chuo Kikuu cha James Paget ambapo upasuaji huo ulifanyika, amesema uchunguzi wa kina ulifanyika juu ya tukio hilo.

“Baada ya tukio hilo, michakato yetu imepitiwa upya, na maboresho yamefanyika katika kila eneo la mahitaji, na tuliyojifunza tumehakikisha yanawafikia wafanyakAZi wetu wote ili kuepuka makosa,” amesema.

Chanzo : Bbc Swahili

Comments are closed.