The House of Favourite Newspapers

Al-Shabaab ni nani? -9

0

AlShabaabfighters014.jpgAl-shabaab wavamia kanisa, kambi ya jeshi, 80 wauawa!

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Wiki iliyopita nilieleza ni kwa jinsi gani Wanamgambo wa Kundi la Al-Shabaab wanavyozidi kuwa tishio la usalama wa raia na mali zao nchini Kenya. Nilionesha ni kwa jinsi gani mataifa makubwa yakiwemo Marekani na Uingereza yalivyoanza kutishika na kuchukua tahadhari dhidi ya balozi zake na raia wake nchini humo. Pia tuliona jinsi ambavyo Al-Shabaab walivyodhibiti eneo kubwa la Somalia la mashambani na kusajili idadi kubwa ya raia wa Kenya. Bado Al-Shabaab wanazidi kuwa tishio kwa Kenya. SONGA NAYO…

Wakati hayo yakiendelea, watu walioshukiwa kuwa ni Wanamgambo wa Al-Shabaab waliripotiwa kuwa walivamia Kanisa la ACK Cathedral lenye maskani yake huko Mombasa ambapo kulikuwa na majibizano makali ya risasi kati ya polisi na magaidi hao.

Katika tukio hilo, polisi walifanikiwa kuwaokoa waumini 100 waliokuwa kanisani wakisali ambapo ghafla kuna gari lilisadikiwa lilifika kanisani hapo likiwa na wanamgambo hao.

Polisi walipofika kanisani hapo walikuta magari yaliyoegeshwa eneo la kanisa, matairi yake yalikuwa yametolewa upepo.

Hata hivyo, katika tukio hilo, hakuna aliyedhurika lakini magaidi hao walikimbia na hawakukamatwa.

Kufuatia tukio hilo, Wakristo nchini Kenya walitangaza maandamano makubwa ya nchi nzima kupinga mashambulio ya Al-Shabaab yaliyokuwa yakiwalenga wao hasa baada ya kushindwa kujibu maswali yaliyohusiana na Dini ya Kiislam.

Wakati hali ikizidi kuwa tete, makomandoo na wanamgambo wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab nchini Somalia, kwa mara nyingine waliripotiwa kuvamia na kushambulia kambi ya kijeshi ya Umoja wa Afrika (AU) nchini Somalia.

Ilielezwa kwamba, Al-Shabaab, wakiwa wamevalia magwanda ya kijeshi, waliua wanajeshi wawili waliokuwa wakilinda amani kutoka nchini Djibouti.

Katika tukio hilo, Kundi la Al-Shabaab lilithibitisha kuvamia kambi hiyo katika Mji wa Bulla Burde, yapata kilomita 200 kutoka Jiji la Mogadishu ambapo lilipambana na wanajeshi hao wa Umoja wa Afrika.

Aliyejitambulisha kuwa Msemaji wa Al-Shabaab, Abdulaziz Abu Musab aliliambia Shirika la Habari la AFP kuwa, Makao Makuu ya Jeshi la Umoja wa Afrika nchini humo yalivamiwa na wapiganaji wa Al-Shabaab na kuua watu wapatao sita.

Kwa upande wake, Msemaji wa Majeshi ya Afrika (AMISOM) nchini Somalia, Elio Yao alikanusha madai hayo ya Al-Shabaab na kusisitiza kuwa, kundi hilo liliwaua wanajeshi wawili wa Djibouti wakati wa mapambano hayo nje ya kambi hiyo.

Alisema kuwa kulikuwa na makabiliano ya risasi katika lango la kuingia kwenye kambi hiyo ambapo wanajeshi wawili kutoka Djibouti waliuawa.

Msemaji huyo alisisitiza kuwa, magaidi hao hawakufanikiwa kuingia katika kambi ya majeshi hayo.

Mashambulizi hayo ndiyo yaliyokuwa makali zaidi kutekelezwa na Kundi la Al-Shabaab dhidi ya wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika nchini humo.

Wakazi wengi wa mji huo walidai kwamba, walisikia milio ya risasi wakati wa mapambano hayo yaliyodumu usiku kucha.

Walisema yalikuwa ni mapambano makali mno yaliyoambatana na milipuko mikubwa kabla ya kupambazuka.

Katika kipindi hicho, mashambulizi makubwa waliyaelekeza kwenye majengo ya serikali lakini Jeshi la Umoja wa Afrika liliapa kushinda vita hiyo.

Jeshi hilo la Umoja wa Afrika lilikuwa likiongozwa na lile la Kenya la KDF ambao kwa pamoja walidaiwa kuwaua zaidi ya wanamgambo 80 wa Al-Shabaab kwenye mapigano yaliyotokea Kusini mwa nchi hiyo.

Ndiyo kwanza mashambulizi ya Al-Shabaab yameshika kasi. Je, nini kiliendelea? Usikose wiki ijayo.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!

Leave A Reply