Al-Shabaab washambulia kambi ya wakimbizi

AlShabaabfighters014.jpgILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Wiki iliyopita nilieleza namna ambavyo Serikali ya Somalia ilivyozituhumu Eritrea na Ethiopia kwa kuwasaidia silaha za kivita kundi korofi na haramu la Al-Shabaab linaloendelea kutekeleza mashambulizi ya ugaidi sehemu mbalimbali katika ukanda huu.

SASA ENDELEA…

Wakati Somalia ikitoa tuhuma hizo nzito, Wanamgambo wa Al-Shabaab waliendeleza mashambulizi yao dhidi ya vikosi vya kigeni nchini Somalia.

Kushamiri kwa mashambulizi hayo kulienda sambamba na kujiunga kwa Jeshi la Ethiopia na vikosi vya kulinda amani vya Afrika nchini Somalia (AMISOM).

Kuhusiana na suala hilo, Msemaji wa Al-Shabaab aliyetambulika kwa jina la Sheikh Ali Mahmoud Rage alikaririwa akisema kuwa, baada ya kujiunga, Wanajeshi wa Ethiopia na vikosi vya AMISOM, viongozi wa Al-Shabaab walikutana na kufanya mazungumzo ya kina kuhusiana na kadhia hiyo.

Katika matukio hayo, viongozi hao wa Al-Shabaab walitangaza kwamba, awali walivishinda vikosi vya Ethiopia hivyo walifahamu kuwa ni juhudi gani walitakiwa kuzifanya ili kuvishinda tena vikosi hivyo.

Askari wa Ethiopia, kwa baraka za Marekani, waliingia nchini Somalia, lakini walilazimika kuondoka baadaye kutokana na upinzani mkubwa walioupata kutoka kwa Al-Shabaab.

Baada ya kuona hali inakuwa tete, kwa mara nyingine, vikosi vya Ethiopia viliingia nchini Somalia. Kuhusiana na suala hilo, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Haile Mariam Dessalegn alitangaza kuwa hakukuwa na sababu ya kuwaondoa askari wa nchi yake nchini Somalia na kwamba, nchi hiyo iliapa kupambana kwa nguvu zote na wanamgambo wa kundi hilo.

Kiongozi huyo alisisitiza kuwa, Wanamgambo wa Al-Shabaab walikuwa ni tishio kwa eneo hilo na kwamba nchi yake kwa kushirikiana na vikosi vya Umoja wa Afrika na askari wa Serikali ya Somalia, waliapa kupambana vikali na tishio hilo kwa gharama na kwa muda wowote.

Katika kujibu mapigo, Msemaji wa Al-Shabaab, Rage naye alifunguka kuwa, hatua ya kujiunga vikosi vya Ethiopia katika oparesheni za vikosi vya Umoja wa Afrika (AU) nchini Somalia, ilionesha udhaifu mkubwa wa kushindwa kwao katika kukabiliana na wapiganaji wa kundi hilo.

Katika oparesheni hiyo, askari wapatao 4,395 wa Ethiopia walijiunga na vikosi vya AMISOM nchini Somalia.

Kujiunga vikosi vingine katika majeshi ya kulinda amani nchini Somalia kulikuja katika hali ambayo watu na mirengo yenye misimamo mikali nchini humo, walikuwa wakipinga uwepo wa vikosi vya kigeni nchini mwao na kutangaza kuwa, kurejeshwa usalama na amani katika nchi hiyo ya pembe ya Afrika kulitakiwa kufanywe na majeshi ya nchi hiyo.

Kwa miaka mitatu mfululizo na kutokana na kupatikana muungano wa kieneo dhidi yao, Wanamgambo wa Al-Shabaab walianza kupoteza ngome zao nchini Somalia na kulazimika kurudi nyuma.

Vikosi vya Umoja wa Afrika (AU) vilifanikiwa kuwavurumusha wapiganaji wa kundi hilo kutoka Mogadishu, Mji Mkuu wa Somalia. Kufuatia ushindi huo, wapiganaji hao wamepoteza pia udhibiti wa miji mingi na vitongoji kadhaa huko Somalia. Katika fremu hiyo, kuondoka katika bandari muhimu ya Kismayu ambayo ni moja ya ngome kuu ya Al-Shabaab, kulikuwa na umuhimu wa aina yake.

Bandari hiyo ilikuwa kituo muhimu cha kupitishia mahitaji ya silaha na chakula kwa ajili ya wapiganaji wa kundi hilo. Katika tahadhari waliyochukua kutokana na pigo walilopata, wapiganaji wa Al-Shabaab walishambulia kambi ya wakimbizi ya Dadaab iliyoko katika mpaka wa Kenya na Somalia na ambayo inahesabiwa kuwa kambi kubwa ya wakimbizi duniani.

Tayari Somalia imeshuhudia mashambulio ya kigaidi ya Al-Shabaab kwenye miji na maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi hiyo.

Kinachoonekana ni kwamba, licha ya vipigo kutoka kwa majeshi ya Afrika, Al-Shabaab wameendelea kukusanya nguvu kwa lengo la kuanzisha mashambulizi mapya dhidi ya majeshi ya nchi hiyo na yale ya kigeni.

Hata hivyo, swali linalojitokeza hapa ni kwamba, kama Eritrea na Ethiopia wanakanusha kuwapa silaha za kivita, je, wanapata wapi silaha za kuendeshea harakati zao na ni nani anayenufaika zaidi na kuendeleza mgogoro nchini Somalia?

Itaendelea wiki ijayo.

Loading...

Toa comment