Al-Shabaab wavamia Chuo Kikuu cha Garissa, waua 147!

AlShabaabfighters014.jpgILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Wiki iliyopita tuliona jinsi ambavyo kulikuwa na mpango wa siri wa kuwasajili vijana kwenye kundi korofi na haramu la kigaidi Afrika Mashariki la Al-Shabaab. Hata hivyo, baadhi ya vijana hao katika eneo la Garissa walikacha baada ya kugundua kuwa walikuwa wamedanganywa. SASA ENDELEA…

Wakati zoezi hilo likiendelea, kuliibuka taarifa nyingine mbaya zaidi ambapo kulitokea Shambulio la Al-Shabaab katika Chuo Kikuu cha Garissa kilichopo Kaskazini mwa Kenya. Taarifa za awali zilionesha kuwa watu wengi wapatao 147 waliuawa kwenye tukio hilo baya lililolaaniwa vikali.

Zoezi la kuokoa wanachuo na watu wengine eneo hilo lilikuwa si la kitoto kwani askari wa Kenya walijikuta kwenye wakati mgumu mno huku wavamizi wanne wa kundi hilo wakiuawa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Serikali ya Kenya, wanavyuo 587 waliokolewa huku 79 wakijeruhiwa vibaya kwenye shambulio hilo la Al-Shabaab.

Majimbo manne karibu na mpaka wa Kenya na Somalia, Garissa, Wajir, Mandera na Tana-River yaliwekwa chini ya uangalizi mkali huku magaidi wengine wakisakwa. Zoezi hilo lilisimamiwa na kamati ya maafa.

Katika tukio hilo, wanafunzi tisa waliokuwa mahututi walikimbizwa kwa ndege katika Hospitali ya Nairobi kwa ajili ya matibabu kunusuru maisha yao.

ILIKUWAJE?

Kwa mujibu wa mashuhuda, watu wenye silaha za moto waliovalia vinyago, walivamia chuo kikuu hicho mapema, majira ya asubuhi.

Hata hivyo, muda mfupi baada ya uvamizi huo, askari wa Kenya waliingia katika eneo la chuo hicho ambapo walinzi wawili walikuwa wamepigwa risasi na kufa papohapo.

Baada ya mashambulizi kati ya askari na Al-Shabaab kupamba moto, wanafunzi walijikuta wakirundikana ndani ya madarasa yao baada ya magaidi wenye silaha kujitawanya kwenye hosteli hasa za wasichana.

Baada ya hali kuwa tete, baadhi ya wanafunzi walitoroka kupitia katika uzio wa chuo hicho kujinusuru.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon alilaani mno uvamizi huo ambao aliuita, ‘uvamizi wa kigaidi’ akisema kuwa UN ilikuwa tayari kuisaidia Kenya, ‘kujilinda na ugaidi huo’.

Umoja huo wa mataifa ulisema utatoa msaada kwa Nairobi ili kupambana na Al-Shabaab na kuendelea kufanya kazi kulishughulikia kundi hilo.

Katika harakati hizo, serikali ya Kenya ilimtangaza Mohamed Kuno, kiongozi wa ngazi za juu wa Al-Shabaab kama mtu aliyepanga shambulio hilo la Chuo Kikuu cha Garissa.

Mtangazaji wa BBC wa Somalia alikaririwa akisema kuwa Kuno alikuwa mwalimu mkuu katika Shule ya Kiislam ya Garissa kabla ya kujitoa mwaka 2007.

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, kwa mara nyingine alitoa salamu za maombolezo kwa familia ya watu walioathirika na ugaidi huo na kuagiza hatua kali za haraka kuchukuliwa mara moja ili kuhakikisha mafunzo ya askari yanatolewa haraka.

Wakati hali ikiwa hivyo, Al-Shabaab walikuwa wakitamba kwamba, wanachama wake walikuwa wakiwashikilia Wakristo wakati Waislam waliwaachia huru.

Hata hivyo, haikujulikana kama waliwaachia na kuwaruhusu kwenda wapi kwani ulipita ukimya bila kujua walikokuwa.

Iliripotiwa kuwa Al-Shabaab waliwaamrisha wanafunzi kujilaza sakafuni lakini baadhi yao walipata mwanya wa kutoroka.

Mwanafunzi, Augustine Alanga alikaririwa akisema: “Hali ilikuwa mbaya mno kwani milio ya risasi ilikuwa ikisikika kila mahali.”

Alisema kuwa, lilikuwa jambo la kushangaza mno kwa chuo kikuu hicho kulindwa na polisi wawili tu.

Naye mwanafunzi mwingine, Collins Wetangula alisema wakati watu wenye silaha wakiingia hosteli, aliwasikia wakifungua milango na kuuliza watu waliokuwa ndani kama walikuwa ni Waislam au Wakristo.

Alisema: “Kwa wale waliojitambulisha kuwa ni Wakristo, walipigwa risasi hadharani na kufa papohapo…”

Al-Shabaab, katika taarifa yao walisema kuwa walikivamia chuo kikuu hicho kwa sababu walikuwa na ugomvi na Kenya.

Itaendelea wiki ijayo.

Loading...

Toa comment