The House of Favourite Newspapers

Al-Shabaab wawatisha Marekani, Uingereza

0

AlShabaabfighters014.jpgILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Wiki iliyopita niliishia pale ambapo Al-Shabaab walikuwa wakiendelea na matukio ya mauaji sehemu mbalimbali nchini Kenya ili kulipiza kisasi wakishinikiza nchi hiyo kuondoa majeshi yake nchini Somalia.

SASA ENDELEA…

Wakati upepo ukiwa haujatulia nchini humo, ghafla kuliibuka habari nyingine mbaya zaidi kuwa takribani watu 36 walikuwa wameuawa katika shambulio la Al-Shabaab lililotokea kwenye machimbo ya kokoto karibu na Mji wa Mandera, Kaskazini mwa Kenya.

Kundi hilo haramu na korofi lilikiri kuhusika na mauaji hayo ya kila kukicha. SASA ENDELEA…

Yalikuwa ni mashambulio bandika bandua! Baada ya mauaji ya machimboni huku Mandera, Kasikazini mwa nchi hiyo, siku chache baadaye maafisa wa polisi wa Kenya walithibitisha kuwa watu 12 walikuwa wameuawa katika mpaka wa nchi hiyo na Somalia.

Katika uchunguzi wao, polisi walidai kuwa shambulio lililoshukiwa kufanywa na Wanamgambo wa Al-Shabaab huku wakiongeza kwamba, katika tukio hilo, watu wengine saba, raia wa Kenya hawakujulikana walipo.

Shambulio hilo lilitokea siku moja tu baada ya jeshi la anga la Kenya kuvamia kwa makombora maeneo yanayoshukiwa kuwa ngome za wapiganaji hao wa Kiislam upande wa Somalia.

Hata hivyo, tofauti na matukio mengine, kundi hilo la Al-Shabaab halikutoa taarifa yoyote kukana au kukiri kuhusika katika shambulio hilo.

Kwa mujibu wa Seneta wa Kaunti ya Mandera iliyoko mpakani mwa Kenya na Somalia, Billow Kerrow, washambuliaji hao walitoka upande wa Somalia na kuja kuvamia eneo lake. Kerrow alisema kuwa ilishukiwa kwamba, jamaa hao walivamia eneo hilo kwa lengo la kujipatia miraa (mirungi) kutoka kwa wafanyabiashara wa zao hilo upande wa Kenya na walipofumaniwa na askari wa Kenya ndipo waliwafyatulia risasi.

Hata hivyo, Seneta Kerrow alikanusha madai hayo kuwa huenda shambulio hilo lilihusika na uhasama wa kikabila na kiukoo ulioko kati ya jamii zinazoishi katika mpaka huo.

Shambulio hilo lilitokea wakati usalama wa eneo hilo ukiwa umeimarishwa nchini Kenya kutokana na tishio la kutokea shambulio la kigaidi dhidi ya maeneo ya umma.

Kufuatia mfululizo wa mashambulizi hayo, ubalozi wa Marekani nchini Kenya ulifikia uamuzi wa kupunguza wafanyakazi wake na kuongeza ulinzi huku Uingereza ikiimarisha usalama katika ubalozi wake na hata kuwaondoa baadhi ya raia wake waliokuwa nchini Kenya kwa usalama wao.

Pamoja na hayo, Wanamgambo wa Al-Shabaab walidaiwa kuzidisha mashambulio nchini Kenya tangu nchi hiyo iingize wanajeshi wake ndani ya Somalia kuwasaka wapiganaji hao haramu tangu mwaka wa 2011.

Wakati zoezi hilo, likiendelea, kwa mara nyingine maafisa wa polisi nchini Kenya waliripoti tukio lingine la mauaji ya watu watatu katika Mji wa Kaskazini wa Wajir yapata kilomita 100 kutoka mpaka wa Somalia.

Watu waliofunika nyuso walishambulia duka moja na kufyatua risasi, kulirushia maguruneti kabla ya kulichoma moto.

Kundi la wapiganaji wa Al-Shabaab lilikuwa limeongeza mashambulizi yake Kaskazini-Mashariki mwa Kenya na kufanya mashambulizi mawili katika Mji wa Mandera ambao unapakana na Somalia.

Kundi hilo linadhibiti eneo kubwa la Somalia la mashambani na limesajili idadi kubwa ya raia Wakenya.

Bado Al-Shabaab wanazidi kuwa tishio kwa Kenya.

Je, nini kiliendelea? Usikose wiki ijayo.

Leave A Reply