Ali Kamwe: Mashabiki wa Yanga ni Mashabiki Wenye Uelewa Mkubwa Kuhusu Soka

Afisa Habari wa Klabu ya Yanga Ali Kamwe amesema mashabiki wa Yanga ni mashabiki wenye uelewa mkubwa kuhusu soka na hata ikitokea kwa bahati mbaya klabu ikashindwa kufuzu kushiriki hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika basi mashabiki hao wataelewa kuwa timu yao ilijitahidi kutimiza adhima.
Ali Kamwe ameyasema hayo wakati akifanya mahojiano ya moja kwa moja na kituo cha Habari cha Global TV na 255Global Radio ambapo amesisitiza kuwa lengo kubwa la Yanga ni kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa kuwatoa klabu ya Al Hilal ya nchini Sudan.

Kwa upande mwingine Afisa Habari huyo ameoneshwa kutofurahishwa na utamaduni wa baadhi ya wasewmaji kuwakejeri wapinzani kwani kwake yeye huo siyo utaratibu wa kazi aliojichagulia na ameweka nia ya kutaka kuiondoa kasumba hiyo kwa ajili ya maendeleo ya mpira wa miguu nchini.
Aidha amesisitiza kuwa ili klabu ya Yanga iweze kufanikiwa kufuzu katika hatua hiyo inawahitaji mashabiki wa klabu hiyo kuiunga mkono klabu yao kwa kununua tiketi na kuingia kwa wingi Uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya Jumamosi ya Oktoba 8, 2022 katika mchezo wa awali wa hatua hiyo ya mtoano dhidi ya Al Hilal ya nchini Sudan.

