The House of Favourite Newspapers

ALI KIBA UNAZINGUA MZEE! USIPOBADILIKA UTAPOTEZA MASHABIKI

Ali Kiba

MWANZONI mwa wiki hii, msanii wa kitambo na mwenye heshima kubwa Bongo, Ali Kiba aliachia video mpya ya wimbo uitwao Hela. Muda mfupi baadaye, video hiyo ilikuwa gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii na mitaani, kila mmoja akizungumza lake lakini wengi walikuwa wakiiponda kwamba haiendani na kiwango cha Ali Kiba.

 

Kabla sijaendelea, nikukumbushe kwamba katika muziki wa Bongo Fleva, kumekuwa na ushindani mkubwa kati ya wasanii wawili wakubwa, Diamond na Ali Kiba kiasi cha kuwagawa mashabiki mitaani, wengine wakiwa wanaamini Diamond ni mkali zaidi ya Ali Kiba na wengine wakiamini kwamba Ali Kiba ndiye mfalme halisi wa Bongo Fleva kama mwenyewe anavyojiita.

 

Ushindani kwa mashabiki ni mkubwa, na pengine kwa sasa, ukiacha ushabiki wa Timu za Soka za Simba na Yanga, na wa vyama vya siasa vya CCM na Chadema, ushindani mwingine unaoongoza kwa kuwagawa watu hasa vijana ni kati ya Team Diamond na Team Kiba. Tofauti ya wasanii hawa wawili, ni kwamba Diamond amekuwa akiwatendea haki mashabiki wake vilivyo, mara kwa mara anaachia ngoma kali zinazobamba si ndani tu ya mipaka ya Tanzania bali mpaka kwenye levo za kimataifa.

 

Kwa Ali Kiba, yeye anaachia ngoma zake kwa msimu, jambo linalowaacha mashabiki wake wakiwa ‘wanyonge’ kwa wale wa timu pinzani, mara kwa mara wanakosa kitu cha kuwatambia wenzao ambao Diamond anawafanya watembee vifua mbele.

Kwa miezi kadhaa Ali Kiba hajaachia ngoma mpya tangu alipoachia Mvumo wa Radi. Juzikati zikazagaa tetesi kwamba yuko kwenye michakato ya kutoa kitu kipya, mashabiki wa pande zote mbili wakakaa mkao wa kula kusubiri kwa hamu kazi mpya.

 

Hata hivyo, matarajio ya wengi yamekuwa tofauti, video iliyotoka ni ya kawaida ukilinganisha na hadhi ya Ali Kiba na kama hiyo haitoshi, wimbo wenyewe siyo mpya. Kwa taarifa yako tu, audio ya wimbo huo ilitoka mwishoni mwa mwaka 2016! Ubora wa video yenyewe siyo ule uliotarajiwa na mashabiki wa msanii huyu katika kipindi hiki cha ushindani mkali.

 

Image result for ally kiba

Baada ya mjadala kuwa mkubwa huko mitandaoni, Ali Kiba aliamua kuufuta wimbo huo Youtube na mpaka naandika makala haya, wimbo huo ulikuwa umefutwa na hakukuwa na sababu zozote zilizotolewa na yeye mwenyewe au menejiment yake, jambo ambalo kwa mashabiki wake, lilikuwa ni pigo kubwa.

 

Zipo taarifa ambazo hazijathibitishwa kwamba kilichofanyika ulikuwa ni mpango maalum (kiki), na kwamba kuna kazi nyingine ambayo ndiyo hasa aliyolenga kuitoa inakuja.

Vyovyote itakavyokuwa, Ali Kiba amewaangusha mashabiki wake kwa sababu ukifuatilia mitandaoni, kinachoendelea ni kwamba mashabiki wa msanii huyo wanashambuliwa wao pamoja na msanii wao kwamba muziki wa ushindani umemshinda Ali Kiba, ni bora aendelee na soka (hivi karibuni alisajiliwa katika Timu ya Coastal Union ya Tanga).

 

Ushabiki wa muziki ni tofauti na ule wa soka au vyama vya siasa, ni rahisi sana shabiki aliyekuwa anampenda sana msanii fulani, kuamua kuachana na msanii huyo na kuanza kumshabikia mwingine endapo ataona ile raha anayoitegemea kuipata, haipati kabisa au hata akiipata, haiji kwa wakati.Kwenye soka mtu anaweza kuvumilia timu yake ikawa inafungwa kila mara lakini akaendelea kukomaa na kuishangilia, kwenye muziki haipo hivyo.

Image result for ally kiba

Kwa jinsi upepo ulivyo kwa sasa, ni lazima Ali Kiba utoke na kuzungumza na mashabiki wako, kama ulipanga iwe kiki, basi wape kile walichokuwa wanakitarajia (kama kweli upo wimbo mwingine tofauti na Hela) lakini pia kama kuna tatizo, ni vyema ukawaeleza ni nini hasa kilichotokea.

 

Kuendelea kukaa kimya, ukiacha mashabiki wako wakiendelea kutukanwa mitandaoni kwa sababu yako, kutawafanya wengi waachane na wewe na waone unazingua kisha. Ni rahisi kuwashawishi watu wakapenda kazi zako, lakini wakishakukatia tamaa, ni ngumu sana kuwarudisha tena na hakuna mwanamuziki bila mashabiki. Take it from me.

Barua Nzito | Na Erick Evarist.

Comments are closed.