The House of Favourite Newspapers

Alibaba Yawatengea Sh. 22 Bilioni Wabunifu wa Tehama Afrika

0
Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Kampuni za Alibaba Jack Ma

 

Baada ya kukamilisha ziara yake nchini Kenya wiki iliyopita, bilionea Jack Ma ametangaza kuanzisha mfuko wa kuendeleza wajasiriamali wa Kiafrika.

Ma ambaye ni mwanzilishi na Mwenyekiti wa Kampuni za Alibaba, alitangaza kutoa Dola 10 milioni za Marekani (zaidi ya Sh22 bilioni ) kwa mwaka,  kwa ajili ya mfuko aliouanzisha ujulikanao kama African Young Entrepreneurs Fund.

“Nataka kuzisaidia biashara za mtandaoni,” alisema Ma ambaye ni mshauri wa Shirika la Dunia la Maendeleo na Biashara (UNCTAD) kuhusu ujasiriamali na biashara ndogo kwa vijana.

“Fedha zipo. Ni zangu, hivyo sina haja ya kuomba kibali cha yeyote kuzitumia,” alisisitiza akibainisha kwamba ataajiri watu wa kuzisimamia na mchakato huo uanze mwaka huu.

 

..akiendesha mkutano wake nchini Kenya.

Kuongeza fursa

Ma alisema atashirikiana na UNCTAD kuwapata vijana 200 wabunifu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), ambao wataenda nchini mwake, kujifunza kutoka kwenye Kampuni ya Alibaba aliyoianzisha 1999 na sasa ina thamani ya Dola 231 bilioni za Marekani (zaidi ya Sh510 trilioni).

Ma aliusema mpango huo alipokuwa kwenye ziara yake ya kwanza barani Afrika.

Amezitembelea nchi za Kenya na Rwanda na mpango huo aliubainisha alipohudhuria mkutano wa Youth Connekt Africa, uliofanyika Jumatatu huko Kigali nchini Rwanda.

Pia, alibainisha nia yake ya kushirikiana na vyuo vikuu vya Afrika kufundisha teknolojia ya intaneti, uundaji wa roboti na biashara ya mtandaoni.

Hata hivyo, alisikitishwa na kukosekana kwa intaneti kwenye baadhi ya maeneo akisema huduma hiyo ni muhimu kuliko ilivyokuwa umeme zaidi ya miaka 100 iliyopita.

 

Jack Ma.

 

Katibu Mkuu wa UNCTAD, Mukhisa Kituyi alisema:

“Wajasiriamali wa Afrika hawatakiwi kuomba au kusambaza bidhaa za mtu bali namna ya kukuza biashara zao au masoko mapya.”

Ma anafuata nyayo za mabilionea wenzake wanaowasaidia wajasiriamali wadogo kama Tonny Elumelu wa Nigeria, anayetoa mikopo kwa biashara zinazochipukia na Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama ambaye ameanzisha Young African Leaders Innitiative (Yali) inayotoa mafunzo na mtaji kwa vijana 500 kila mwaka.

Vijana hao hupelekwa Marekani ambako hupatiwa mafunzo ya ujasiriamali na uongozi.   

Leave A Reply