The House of Favourite Newspapers

ALICHOFANYIWA MTOTO HUYU… MATIBABU INDIA UTATA WAIBUKA!

WAGONJWA wengi wakiambiwa wanapelekwa nchini India kwa ajili ya matibabu, husema; “Asante Mungu” wakiamini huko ndiko uliko uponyaji, kumbe sivyo, Risasi Jumamosi lina stori ya matibabu India kuibua utata.  

 

Mwaka 2013, kijana Hamis Hashim Liguya (miaka 19 mwenye picha ukurasa wa mbele), mkazi wa Yombo-Dovya jijini Dar, anayeteseka na uvimbe kwenye miguu yake alipoambiwa anapelekwa India kutibiwa, alifarijika, lakini leo faraja yake imetoweka kabisa. Imetoweka kwa sababu hata baada ya kutumia fedha nyingi kwenda nchi hiyo ya ng’ambo kutafuta tiba, alichorudi nacho, sicho alichotarajia.

 

UFAFANUZI PICHA ZA UKURASA WA MBELE

Katika ukurasa wa mbele wa gazeti hili, kuna picha tatu za kijana Hamis; ya kwanza kushoto inamuonesha alipokuwa anaumwa kabla ya kupatiwa matibabu, huku ya katikati ikiwa ni baada ya kutibiwa India. Pengine picha hizo mbili zinaweza kuonesha hali tofauti, lakini ile ya tatu kulia ambayo inaonesha hali aliyonayo sasa ndiyo iliyoibua utata wa matibabu yatolewayo nchini India miongoni mwa wengi.

 

PATA KIDOGO HISTORIA YA UGONJWA WA HAMIS

Tatizo la Hamis lilianza baada ya kuteguka mguu wake wa kulia, akiwa na umri wa miaka mitano na baadaye wazazi wake waliangaika kutafuta namna ya kumtibu katika hospitali za ndani ya nchi, lakini ilishindika. Kutokupona kwa mguu wa Hamis kunatajwa na madakrati kuwa kulichangiwa na udhaifu wa mifupa yake.

 

Mwaka 2013, kwa msaada wa wasamaria wema, kijana Hamis alifanikiwa kupelekwa India kwa matibabu ambako wataalam walishauri mguu wake wa kulia ukatwe. Hata alipokatwa mguu na kupatia tiba kwa mujibu wa madaktari wa Hospitali ya Apollo, Hamis hakupata uzima aliotarajia badala yake alipata nafuu na baadaye mateso kumrudia mara kumi zaidi. Miaka mitano tangu afanyiwe matibabu India ugonjwa wa Hamis wa mguu kuvimba na kujaa maji umekomaa kiasi cha kufikia uvimbe kuwa na uzito unaokadiriwa kuwa na kilo 50.

 

UTATA WA MATIBABU INDIA WAIBUKA

Uhusiano kati ya Serikali ya Tanzania na Hospitali za Apollo nchini India ulianza mwaka 2004 ambapo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iliingia makubaliano rasmi (Memorandum of Understanding) na katika makubaliano hayo, wagonjwa kutoka nchini wanaogharimiwa na Serikali hupelekwa katika hospitali hizo kwa ajili ya matibabu ya rufaa.

 

Yapata miaka 14 tangu makubaliano hayo yafikiwe, imani ya wagonjwa wa Tanzania kutibiwa India imekuwa kubwa; lakini siku za hivi karibuni baadhi ya watu imani zao zimeanza kushuka.

Kushuka kwa imani kumetokana na kuwepo kwa kesi nyingi mfano wa ile ya Hamis ya baadhi ya Watanzania kutibiwa India na kutopona. Ifahamike kwamba hospitali zenye mkataba na Serikali ambazo zimekuwa zikiaminika kwa tiba makini ni nyingi zikiwemo za Indraprastha Apollo, New Delhi, Apollo Chennai, Apollo Hyderabad, Apollo Bangalore, Apollo Ahmedabad, Apollo Kalkata na nyinginezo.

 

JE, MAADILI DHAIFU YA TIBA YAMEINGIA INDIA?

Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya huduma za jamii barani Afrika hususan afya wanasema kinacholifanya bara hili kukosa tija kwenye suala la matibabu ni udhaifu wa maadili kwa watoa hutuma. “Unaweza kuwa na vifaa vya kisasa kabisa vya matibabu, lakini watoa hutuma wakiwa dhaifu kwenye maadili huwezi kupata matokea chanya.

 

“Mimi nafikiri naweza kuwa sahihi au la kwamba hata India kunaweza kuwa kumeingiliwa na ‘kansa’ ya watoa huduma kuwa na maadili dhaifu. “Nasema hivi kwa sababu kesi za watu kufia India, kurudi wakiwa hawajapona zimekuwa nyingi tofauti na zamani nadhani kuna shida, nasema tena nadhani,” alisema Dk Adrew Peter, mkazi wa Temeke, Dar aliyewahi kufanya kazi Hospitali ya Muhimbili miaka ya 80 kabla ya kustaafu.

 

HUDUMA ZA AFYA NI MAPATO

Katika nchi nyingi zenye mafanikio kuhusu masuala ya afya zimekuwa zikiichukulia huduma ya matibabu kuwa vyanzo vikuu vya kukuza uchumi wao. Nchi kama India imekuwa ikinufaika kwa kiwango kikubwa na mapato yatokanayo na wageni kutoka nchi mbalimbali hasa za Afrika kuingia nchini humu kufuata tiba.

 

Kwa mfano; kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2014/15 inaonesha kuwa madeni ya Serikali katika hospitali za rufani za India ni Sh. 27,800,677,740. Kiasi hicho cha fedha ni ongezeko la Sh. 10,860,284,536 kulingana na madeni ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2013/14 katika Hospitali za India, ambayo yalikuwa Sh. 16,940,393,204.

 

Kwa mujibu wa ripoti ya CAG iliyowasilishwa bungeni katika mwaka wa fedha 2014/15, Hospitali ya Apollo Hyderabad ilikuwa inaidai Serikali ya Tanzania shilingi bilioni 4.831. Wakati Hospitali ya Apollo Chennai ilikuwa inadai shilingi bilioni 8.687. Hospitali ya Apollo Bangalore inadai shilingi bilioni 1.245, Apollo Ahmedabad, inadai shilingi bilioni 1.906, Apollo Newdelhi inadai Sh. bilioni 10.117 huku Madras Medical Missioni ikidai Sh. bilioni 1.014.

 

Hizi ni fedha nyingi ambazo Serikali ya India ilivuna kutokana Tanzania kupeleka wagonjwa wake kutibiwa nchini humo. Takwimu kutoka Ofisi ya Mwambata wa Afya katika Ubalozi wa Tanzania nchini India zinaonesha kuwa kwa miaka mitatu Watanzania takriban 25,000 waliomba visa (tamka viza) kuingia nchini India kwa ajili ya kupata matibabu.

 

TIBA KUTOLEWA ILI KUPATA FEDHA?

Kumekuwa na hofu miongoni mwa wananchi wengi kwamba hospitali nyingi hasa za binafsi zimekumekuwa zikitoa tiba kwa lengo la kupata fedha na si kutibu wagonjwa. “Mimi nilishaacha siku nyingi kutibiwa kwenye hizi hospitali, nyingi zipo kwa ajili ya kupata fedha na si kutibu.

 

“Ukifika hospitali unaambiwa magonjwa mengi ili tu utoe fedha nyingi, hata huko nje siku hizi nako kumeharibika watu wanatibiwa ili waache hela siyo wapone matatizo yao. “Wangapi wamekwenda nje ya nchi kutibiwa na kurudi kufia hapa Tanzania,” aliandika Ashura Juma katika ukurasa wake wa Facebook alioambatanisha na picha ya marehemu Mzee Majuto.

SERIKALI YATAKA WATANZANIA WATIBIWE NCHINI

Kwa miaka mingi kumekuwa na wimbi la Watanzania hasa viongozi kuomba kutibiwa nje ya nchi, jambo ambalo Rais John Pombe Magufuli katika uongozi wake amewataka Watanzania waachane na mazoea ya kutibiwa nje ya nchi, badala yake watumie hospitali za ndani kutibu matatizo yao. Mara kadhaa amekuwa akisisitiza kuwa magonjwa yaliyokuwa yakilazimisha wagonjwa kutibiwa nje sasa yanatibiwa hapa nchini.

 

Magonjwa ambayo yameongoza kuwapeleka Watanzania nchi ya nchini ni pamoja na moyo, figo na saratani ambayo kwa sasa yote yanatibiwa kwa ufanisi mkubwa katika hospitali za ndani hasa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete –Muhimbili ambayo kwa sasa imeimarisha huduma zake kwa kiwango cha juu.

 

TUREJEE KWA HAMIS

Hamis ambaye anaishi kwa shida licha ya kutibiwa India na kuteketeza kiasi cha shilingi milioni 20 na kutopata nafuu amezidi kuwaomba wasamaria wema wajitokeze kumsaidia ili aweze kuutibu ugonjwa unaomsumbua.

“Sasa hivi ninaishi maisha ya kuombaomba watu pale Gerezani-Kariakoo ambako ili nifike huko kila siku kuomba natakiwa kuwa na shilingi elfu 30 kwa ajili ya Bajaj. “Yaani nataabika sana, naomba mtu au taasisi inayoweza kunisaidia, inisaidie nimechoka na haya mateso,” alisema Hamis.

 

KWA NINI UGONJWA HUJIRUDIA?

Daktari maarufu jijini Dar, Godfrey Chale aliliambia Risasi Jumamosi kuwa watu wengi ambao hurudiwa na matatizo yao husababishwa na kutozingatia ushauri wa daktari.

“Kuna mgonjwa anaweza kufanyiwa upasuaji, akaambiwa arejee hospitali baada ya mwezi au miezi kadhaa, lakini harudi, unategemea nini? “Kuna mwingine anapewa masharti baada ya kutibiwa kwamba asifanye hivi na vile au afanye hili na lile ili tiba ikamilike, lakini wagonjwa wengi hawatekelezi maelekezo wanaopewa, wakiona wamepata nafuu kidogo wanapuuza tiba, matokeo yake ndiyo hayo ya ugonjwa kukomaa zaidi ya mwanzo.

Comments are closed.