The House of Favourite Newspapers

Alichokisema Mo Dewji Baada ya Kuibuka Msikitini

MAMBO sasa ni safi ndani wa Simba! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya mwekezaji mkuu wa klabu hiyo, Mohamed Dewji ‘Mo’ kujitokeza hadharani kwa mara ya kwanza tangu alipoachiwa huru kutoka mikononi mwa watekaji.

 

Hivi karibuni Mo alikumbwa na balaa la kutekwa na watu wasiojulikana wakati alipokuwa akiingia katika Gym ya Hoteli ya Colessium iliyopo jijini Dar es Salaam na alikuja kuachiwa huru baada ya kupita siku tisa ambapo alitelekezwa maeneo ya Gymkhana jijini Dar.

 

 

Jana Mo alijitokeza hadharani kwa mara ya kwanza tangu aachiwe huru baada ya kwenda kufanya ibada ya Swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Sinashiri uliopo Mtaa wa Indira Gandhi, Upanga jijini Dar es Salaam. Akiwa msikitini hapo, Mo aliwashukuru waumini wa msikiti huo na Watanzania wote kwa ujumla kwa dua zao walizokuwa wakimwombea ili aweze kutoka salama mikononi mwa watekaji hao.

 

“Hilo ndilo jambo kubwa ambalo kiongozi wetu huyo alienda kulifanya msikitini hapo ambapo ndipo huwa anaswali. “Lakini pia baada ya kutoka msikitini alitoa sadaka ya shukurani kwa baadhi ya watu waliokuwa msikitini hapo kisha akaondoka zake akiwa ameambatana na baadhi ya ndugu zake wa karibu,” alisema kiongozi wa Simba ambaye aliomba hifadhi ya jina.

 

Hata hivyo, baada ya taarifa hizo, gazeti hili lilimtafuta Mo kwa njia ya simu ili aweze kuzungumzia suala hilo hakupatikana kama ilivyokuwa pia kwa msemaji wa familia hiyo, Azim Dewji ambaye yeye simu yake ilikuwa ikiita tu bila ya kupokelewa.

 

Mjumbe wa Kamati ya Simba, Said Tully alithibitisha kuwa dua hiyo ilikuwa maalum kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa Mo kutoka mikononi mwa watekaji na ilihudhuriwa na mashehe, wachungaji, wafanyabiashara pamoja na baadhi ya wadau wa soka. “Kwa upande wa viongozi wa Simba, nilihudhuria mimi pamoja na kaimu rais (Salim Abdallah ‘Try Again’),” alisema Tully.

Comments are closed.