The House of Favourite Newspapers

Aliens akamatwa, ahifadhiwa!

0

Scary_Movie_AliensWiki iliyopita nilizungumzia eneo hatari linaloaminika kuwa ni makao ya Aliens au makao makuu ya shetani hapa duniani. Ni Bermuda Triangle inayopatikana Pwani ya Kusini-Mashariki mwa Marekani na ipo katika Bahari ya Atlantiki. Nilieleza ni kwa jinsi gani eneo hilo limepakana sana na Visiwa vya Caribbean na hukabiliwa na upepo mkali na wingu zito ambavyo husababisha mushkeli kwa ndege, meli na binadamu huku Aliens wenyewe wakidaiwa kupeta kwa raha zao.

SASA ENDELEA…

Baada ya kuiona Bermuda Triangle na sarakasi zake, kuna eneo lingine hatari zaidi duniani ambalo ni la siri sana. Hili eneo linajulikana kwa jina la Area 51. Niliwahi kudokeza kwenye matoleo yaliyopita na sasa tunaliangalia kwa undani sana.

Eneo hili linalohusishwa na hawa viumbe wa ajabu waishio angani wa Aliens lipo nchini Marekani katika Jimbo la Nevada. Inawezekana eneo hili likawa na sarakasi nyingi hata kuliko Bermuda Triangle.

Eneo hili ndipo kulipo kituo kikuu cha ujasusi cha Marekani. Inaaminika kuwa majasusi wa Marekani hukutana na Aliens na kushirikiana siri na maarifa ya kisayansi ya jinsi gani ya kuitawala dunia.

Ni eneo hilihili ambalo linadaiwa kuwa kuna Aliens amehifadhiwa katika kituo hicho baada ya kukamatwa na majasusi wa Marekani miaka ya 90. Inasemekana kwamba Aliens huyo alikamatwa baada ya kuachwa na wenzake waliotorokea angani na kumsahau mwenzao mmoja aliyekuwa mbali na kuishia mikononi mwa majasusi wa Marekani ambao baada ya kumkamata walimuhifadhi.

Mbali na majasusi hao, si rahisi kwa mtu wa kawaida kuingia kwenye eneo hilo la jeshi hata watawala wa Marekani huingiza ndani ya kituo hicho kwa kiapo maalum na hutokea mara moja kwa miaka 10.

Katika eneo la Area 51, inasemekana kuwa viumbe hao walianguka mahali hapo baada ya kuikaribia dunia wakiwa na chombo chao cha UFO (Unidentified Flying Object). Baada ya kuanguka, walipokuwa wanapaa waliacha mabaki ya chombo hicho yaliyochukuliwa na majasusi hao na inasemekana kuwa teknolojia yote ya Mmarekani imetokana na viumbe hao.

Kwa mujibu wa watu waliokishuhudia chombo hicho kikiwa angani wakati kinashuka eneo hilo, walisikia mlipuko na kishindo kikubwa na baada ya kuanguka walikwenda kukiangalia lakini walipofika nje ya kituo hicho walikuta kila kitu kimeshachukuliwa kwa haraka na kuhifadhiwa na majasusi hao.

Inaelezwa kwamba zoezi hilo lilifanywa kwa haraka mno na kwa siri kubwa ndani ya eneo hilo la Area 51.

Kuna madai mazito kwamba, hata zile simulizi za kwamba Marekani ndilo taifa la kwanza kutua kwenye mwezi, ni video tu na kwamba zilirekodiwa ndani ya Area 51 lakini huwa ni vigumu kupata ushahidi kwa sababu eneo hilo lina ulinzi wa hali ya juu. Ili kupata ramani kamili au undani wa hiki ninachokieleza unaweza kutazama kwenye Google japokuwa eneo hilo ni jangwa kubwa, lakini majengo ya kituo hicho yanaonekana.

Kuna maelezo kuwa ukweli ni kwamba, vitu vingi wanavyofanya majasusi hao siyo akili za kibinadamu, inasemekana wanapewa na Aliens ambao wana uwezo wa kuishi hadi miaka 10,000.

Pia eneo hilo ambalo serikali ya Marekani hulitengea bajeti kubwa inasemekana lilitengwa na kujengwa maalum kwa ajili ya kutengenezea na kujaribu silaha za kijasusi hasa za angani. Ndege kama B12 na F117 ni mazao ya Area 51 likiwa chini ya majasusi wa CIA na NASA.

 

Itaendelea wiki ijayo.

 

Leave A Reply