The House of Favourite Newspapers

Aliens ndiyo vibwengo kwa Afrika?

AliensIILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Kama nilivyoeleza mwanzoni wakati naanza simulizi hii, katika uumbaji, Mungu aliumba viumbe wanaoonekana na wasioonekana. Kuna uwezekano kuwa wasioonekana ni wengi kuliko wanaoonekana.

Mpenzi msomaji wiki iliyopita tuliona kuwa kuna uwezekano mkubwa wa hawa viumbe wa ajabu waishio angani wa Aliens kuishi kwenye Sayari ya Mars kutokana na uwepo wa maji na mabaki ya viumbe wenye makazi kwenye sayari hiyo. Ikumbukwe kwamba popote penye maji kuna uhai. SASA ENDELEA…

Miaka nenda rudi iliyopita, kumekuwa na simulizi nyingi za kutisha mno za viumbe au vitu ambavyo hujitokeza ghafla angani na kusababisha mshtuko kwa binadamu. Mara nyingi vitu au viumbe hawa huwa ni vigumu kuelezea kutokana na kutokea kwake ambako huwa ni kwa spidi kali ya ajabu ambayo binadamu hana.

Lakini wanasayansi na wataalam wa anga duniani wanakiri kwamba, kwa sasa mauzauza ya angani hasa sarakasi za Aliens zimepungua ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Zipo sababu mbalimbali ambazo wanasayansi wameibuka nazo kuwa kupungua kwa sarakasi za Aliens kunatokana na kuongezeka kwa ustaarabu wa binadamu.
Inaelezwa kuwa Aliens walikuwa wakivamia duniani hasa katika kipindi ambacho kulikuwa na shida ambapo kulihitajika nguvu ya ziada kutoka nje ya dunia ili kutatua tatizo hilo.

Aliens waliaminika kuwa walikuwa wanawapa binadamu ujuzi wa ziada juu ya majira kwa kufuata nyota na hesabu. Ndiyo maana katika ulimwengu wa kisasa wa 3D yaani mtazamo wa sayansi ya kifizikia na kifalsafa ndiyo hali inayowafunga binadamu kushindwa kusafiri kwenda kuiona kesho na kurudi nyuma kuiona jana.

Sasa katika ulimwengu huo, kuna tetesi kuwa hawa Aliens wameingia mikataba na mataifa makubwa kama Marekani na Urusi kushirikiana katika teknolojia. Inaelezwa kuwa ushirikiano huu umesaidia mno kukua kwa teknolojia kwa kipindi kifupi kuliko muda wowote wa mwanadamu kuishi duniani.

Lakini mjadala mkubwa umekuwa ni kwa nini ushirikiano huo umekuwa ukihusishwa zaidi na mataifa ya Magharibi katika siku za hivi karibuni?

Jibu la swali hili ni rahisi sana kuwa ni kwa sababu mataifa ya Magharibi hupendelea kufuatilia na kutafiti kiuchokozi tofauti na mataifa mengine ambayo hayajafanya utafiti wa kutosha wa anga.

Katika miaka ya 90 Wizara ya Ulinzi ya Uingereza iliunda tume maalum ya kutathmini viumbe hawa na umuhimu wake katika ulinzi wa anga.

Kwa upande wa Afrika, inawezekana wapo viumbe kama hawa lakini mara nyingi wamekuwa wakihusishwa na mambo ya ushirikina kutokana na elimu ndogo ya sayansi na teknolojia.

Inawezekana ni kweli hawa Aliens wapo ila kumekuwa na mitazamo mbalimbali juu yao tofauti na mataifa ya Magharibi ambao wamekuwa wakiripoti kuwashuhudia viumbe hao kutoka sayari nyingine.

Barani Afrika wapo wanasema Aliens ni viumbe waitwao Vibwengo ambao ni aina ya viumbe waliojazia kama Pawa Mabula, wana misuli hatari lakini wafupi kama kistuli.
Wengine wamewapa majina kama Kinyamkera, Maimuna na vitu kama hivyo.

Hata hivyo, watu hawashughuliki kujua ni nini wameona na kwa nini wameona na walichokiona ni kutoka wapi kwa kuwa tayari wanajua walichokiona ni Kibwengo hivyo anachofanya ni kukimbilia kanisani aombewe au kwa mganga azindikwe.

Wengi waliosoma shule za bweni Tanzania na waliowahi kufika maeneo yaliyotelekezwa kwa muda mrefu kwa namna moja au nyingine wamewahi kusikia kuhusu mtu fulani au watu fulani kushuhudia kiumbe wa ajabu asiye binadamu au chombo cha ajabu kikitembea ardhini au kikipaa au kushuka kutoka angani. Wengi huhusisha na mambo ya kishirikina.

Itaendelea wiki ijayo.

Comments are closed.