The House of Favourite Newspapers

Aliens waonekana Palestina, Israel, Iran na Australia!

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Mpenzi msomaji wiki iliyopita nilieleza kwa kina ni kwa jinsi gani viumbe wa ajabu wa Aliens walivyoliteka anga la Mexico kwa mgongo wa UFO. Tuliona kuwa Julai 11, 1991, watu wapatao 17 ambao hawakuwa na uhusiano wowote katika maeneo tofauti nchini humo, wakiwa na kamera zao, walinasa picha ya sinia kubwa la chuma karibu kabisa na usawa wa jua ambalo muda mfupi nyuma lilikuwa limepatwa. Sinia hilo lilikuwa limening’inia angani kwa muda bila kusogea upande wowote ule.

Walionasa tukio hilo hawakujua kama wamepiga picha UFO mpaka watu wengine walipong’amua wakati wanaoneshwa video hizo.

SASA ENDELEA…

Baada ya tukio hilo lililovuta hisia za wengi na mjadala mkubwa, ndipo watafiti wa Mexico wakaanza kupokea video na picha nyingi zilizoonesha umbo la duara kubwa la chuma, UFO zikiwa kwenye anga la Mexico ambazo picha zake zilipigwa na watu binafsi.

Wapo marubani kadhaa walioripoti kuviona vyombo hivyo vikivinjari katika anga la Mexico.

Kuanzia hapo nchi ya Mexico imekuwa na historia ndefu ya kuonekana kwa UFO na viumbe hao katika anga lake. Wapo baadhi ya wanasayansi ambao wamekuwa wakidharau vyombo hivyo kwa madai kwamba ni vipande vya uchafu tu au vumbi kutoka kwenye anga, roketi za kivita, maputo ya hali ya hewa au uzushi tu.

Kwenye moja ya magazeti ya Mexico la Januari 2, 1993 na vyombo vingine vya habari viligubikwa na habari moja tu ya chombo kisichofahamika na chenye tabia zisizolingana na chombo chochote kinachojulikana na wakazi wa duniani. Chombo hicho kilibaki kwenye anga la Mexico kwa saa tano. Gazeti moja kubwa la Mexico la La Prensa lilikuwa na kichwa kikubwa cha habari, ‘MAAJABU! UFO kwenye anga la Mji Mkuu’. Tukio hilo pia lilirekodiwa na rada kutoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mexico.

Mmoja wa watafiti wa masuala ya UFO, Brit Elders alipokuwa akizungumzia tukio la UFO kunasa kwenye rada za Mexico alikaririwa: “Rada za Mexico zimefuatilia na kurekodi UFO sawa na yale yanayosemwa na watu waliyoona kwa macho yao wenyewe kutoka aridhini na kutoka kwa marubani wa ndege wakiwa angani.

Serikali ya Mexico iliposhinikizwa kulifanyia uchunguzi suala la UFO, ilifanya mkutano na waandishi wa habari kutambua juu ya kuonekana kwa vyombo hivyo lakini ikasema –UFO hazina madhara yoyote kwetu sisi binadamu hivyo hatupaswi kuwa na hofu yoyote.

Kuhusiana na UFO na Aliens, tukiachana na Mexico tunaelekea kwenye Dola ya Palestina ambako Septemba 17, 1996, Kituo cha Polisi cha Tel Aviv nchini humo kilipokea simu za kumwaga kutoka kwa wakazi ambao waliona chombo chenye mwanga mkali kikizunguka kwenye anga lao kwa namna ambayo hakuna ndege wala helikopta ambayo ingeweza kufanya kitu kama hicho.

Mwaka 1997 kwenye mahojiano na Jarida la British Journal UFO Reality kulikuwa na makala kuhusiana na kile kilichotokea kwenye ardhi ya nchi hiyo.

Ilisomeka: “Vyote kwa pamoja (Aliens na UFO) vimeanza kuonekana kwenye anga la Israel, Iran na Australia kwa wakati mmoja.

“Agosti mwaka 1996, wimbi la mashahidi waliona kwa macho UFO na haikuwa watu wa kawaida peke yao kwani hata maofisa wa polisi na jeshi. “Taarifa zilizopokelewa ni nyingi na zilikuwa zikiongezeka siku hadi siku na hata kuwa ni vigumu kuweka taarifa ya mtu mmojammoja.”

Ukweli ni kwamba tukio hilo lilishuhudiwa na maelfu ya watu ambao waliona UFO ikisafiri taratibu mita 200 kutoka ardhini. Vituo vya polisi na vya dharura vilipokea simu za kutosha kutoka kwa watu waliotaka kujua kulikoni na wengine wakishuhudia kuyaona hayo. Ilikuwa ni usiku wa manane, watu walisimama na kutazama UFO kama kitu kikubwa mno kilichokuwa na taa na mwanga wa kutosha kumulika anga la vitongoji viwili kwa mpigo.

Tukio hilo lilishuhudiwa kwa takriban dakika kumi, halafu ghafla, bila tahadhari yoyote chombo hicho kikatoweka kwenye macho ya watazamaji wake.

Sarakasi za viumbe hawa wa ajabu zinazidi kusambaa duniani. Je, nini kitaendelea? Usikose wiki ijayo.

Itaendelea wiki ijayo.

Leave A Reply