The House of Favourite Newspapers

ALIKIBA Msikilize Mzee wa Upako, Ana Hoja!

Ally Salehe Kiba ‘Alikiba’

KWAKO mkali wa Bongo Fleva, Ally Salehe Kiba ‘Alikiba’. Mambo ni vipi? Uko poa? Unaendeleaje na mishe za kila siku?

 

Hongera sana kwa idea yenu ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kusapoti elimu mliyoifanya wewe na Samatta. Ni jambo zuri na la kupongezwa, mmeonesha mfano wa kuigwa kwa wenzenu.

Ukitaka kujua afya yangu, mimi ni mzima bwana. Namshukuru Mungu naendelea kulisongesha ndani ya jumba la magazeti Pendwa, Global Publishers.

 

Nimekukumbuka leo kwa barua. Unajua kutokana na ubize wa majukumu yetu, yawezekana tukamaliza hata mwaka hatujaonana lakini kwa vile uwanja huu upo, ni vyema nikautumia ili kuweza kukueleza kile ambacho kipo moyoni mwangu.

Kiba wewe ni miongoni mwa mastaa wakubwa Bongo, heshima yako ni kubwa hivyo unapaswa kuwa makini kwa kile ambacho kimekuwa kikisemwa hususan katika suala zima la majivuno. Naweza nikasema pia ni kama unajisikia flan hivi.

 

Hili la kujisikia yawezekana si geni sana kulisikia likielekezwa kwako kwa maana watu mbalimbali wamekuwa wakikusema hivyo huna budi kulifanyia kazi. Katika maisha kuna njia nyingi za kupita lakini wengi wanaofanikiwa ni wale ambao wamekuwa na desturi ya kujishusha.

Majivuno ni dalili ya kujisikia, ni ishara ya kuonesha una dharau. Kuwadharau wengine si jambo jema. Hata katika vitabu vya dini tunafundishwa kujishusha. Acha watu wakukweze lakini wewe jishushe kwao. Unapojishusha ndipo utakwezwa na Mungu.

 

 

Nilimsikia Mchungaji Anthony Lusekelo ‘Mzee wa Upako’ katika moja ya mahojiano yake aliyoyafanya hivi karibuni, alipoulizwa kuhusu wasanii wakubwa wawili Bongo, Nasibu Abdul ‘Diamond’ na wewe, alisema mwenzako ni msikivu, mnyenyekevu lakini wewe akasema unajisikia.

Alibainisha wazi kwamba hata ukiwa kwenye mahojiano, akasema ukiwa wewe na Diamond katika mahojiano, wewe utajibu kwa majivuno, lakini mwenzako atajibu vizuri, hilo kwako ndio tatizo.

 

Kwenye eneo hilo, sitaki kusema kwamba umsikilize kwa kuwa yule ni mchungaji, la hasha! Umsikilize tu kama mtu aliyekuzidi umri. Achana na mambo yake mengine yote lakini wewe shika ile kauli yake tu ya kwamba wewe unajiona.

Ameliona jambo hilo kwako. Unapaswa kulifanyia kazi. Unaweza kuona kuna mambo hayaendi vizuri kwako kwa sababu tu ya kutojishusha kwa watu. Kutojinyenyekeza kwa watu. Kujiona wewe ni bora kuliko wengine, kuwa na maringo ni mambo yasiyofaa haswa kwa wewe ambaye unahitaji zaidi watu.

 

Wewe ni mfano, wewe ni kioo cha jamii na hakuna mtu ana shaka na uwezo wako katika muziki hivyo una kila sababu ya kuweka sawa eneo hilo na naamini wewe ni msanii mkali Bongo. Jirekebishe kaka, mambo utaona jinsi yanavyonyooka kwako endapo utajishusha. Nikutakie mabadiliko mema na mafanikio zaidi, kila la kheri kaka!

Mimi ni ndugu yako;

Erick Evarist

Comments are closed.