The House of Favourite Newspapers

Alikufa Vita Taifa, Mazembe Atapigwa Tu

KWA mara nyingine jana usiku Caf iliirudisha tena Simba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya droo ya hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Simba itaanzia mechi yake ya kwanza nyumbani dhidi ya TP Mazembe ya Kinshasa.

 

Awali kwenye hatua ya makundi Simba ilikwenda Kinshasa kucheza na AS Vita ya huko ambako ilipigwa mabao 5-0 kwenye mchezo wa kwanza lakini kwenye marudiano ikashinda bao 2-1 Jijini Dar es Salaam.

Kwenye hatua hii ngumu ya mechi mbili za ugenini na nyumbani zinazozingatia uwiano wa pointi na mabao, Simba itacheza mechi yake ya kwanza nyumbani Ijumaa ya Aprili 5 jioni. Mechi ya marudiano ambayo itaamua nani afuzu nusu fainali itapigwa Jijini Kinshasa Ijumaa ya Aprili 12.

Kikosi cha AS Vita wakiwa katika Uwanja wa Taifa.

Mara ya mwisho Simba kukutana na Mazembe ilikuwa msimu wa 2011 kwenye mashindano hayo ambapo Simba ilipigwa nyumbani na ugenini lakini ikawauzia Mazembe wachezaji wake kadhaa akiwemo Mbwana Samatta na Patrick Ochan. Kwenye mechi ya Dar es Salaam, Simba ilipoteza mabao 2-3 lakini ugenini ikajikuta ikifungwa mabao 3-0 na kutolewa mashindanoni.

 

Kwenye Uwanja wa Taifa, Simba ina rekodi nzuri kwani hatua ya makundi haikupoteza mchezo hata mmoja ikizipiga JS Saoura, Al Ahly na AS Vita. Lakini ilipokwenda ugenini ikapoteza michezo yote mitatu kwa idadi kubwa ya mabao.

 

Simba inakwenda Kinshasa ikilazimika kupambana na mashabiki wa Vita ambao bado wana kinyongo nao na ukumbuke kuwa sasa Vita ni wakali kuliko Mazembe.

 

Kabla Vita hawajaja hapa nchini walikuwa wamewachapa Mazembe mabao 3-0 na hivyo ni rahisi kuwaambia Mazembe kuwa kama Vita walikufa hao ni nani?

Comments are closed.