The House of Favourite Newspapers
gunners X

Anayedai Kubuni Jina Tanzania Amwomba JPM Msaada

MTANZANIA anayedai alishikiri shindano la kubuni jina ‘Tanzania’ kwa ajili ya Jamhuri ya Muungano mwaka 1964, Jotham Chagwah, amemwandikia barua Rais John Magufuli, akimwomba kutambua mchango wake katika ubunifu wa jina la taifa.

 

Chagwah ni mkufunzi mstaafu wa Chuo cha Ualimu Marangu kilichoko Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro ambaye kwa sasa anaishi  Mtaa wa Kilototoni ulioko Mamlaka ya Mji Mdogo wa Himo.

 

“Mwaka 1964 wakati nikiwa nasoma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Tanga, nilishiriki shindano la kubuni jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya Tanganyika na Zanzibar kuungana.

 

“Wakati shindano hilo likiendelea, serikali iliahidi kutoa zawadi ya Sh. 200 kwa mshindi wa shindano hilo na mimi nilibahatika kuwa miongoni mwa washindi na kutumiwa Sh. 12.50 kwa hundi iliyopitia kwa mkuu wangu wa shule niliyokuwa nasoma,” alisema.

 

Kutokana na ushindi huo, Chagwah amesema amewandikia barua Rais Magufuli kumwomba kutambua mchango wake huo ili apewe heshima yake kama mmoja wa watu wazalendo.

 

Katika barua yake hiyo, Mtanzania huyo amemweleza historia yote namna alivyoshiriki shindano hilo baada ya Serikali ya Tanganyika na Zanzibar kutoa tangazo la kuwataka wananchi washiriki.

 

Baadhi ya viongozi wa kisiasa, akiwamo Felista Mtui ambaye ni Diwani wa Viti Maalum katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, aliishauri serikali kujenga utamaduni wa kuzitambua juhudi zilizofanywa na wananchi wake, kabla na baada ya uhuru ili kuweka kumbukumbu sahihi kwa faida ya vizazi vijavyo.

Comments are closed.