The House of Favourite Newspapers

ALIYEDAI KUCHOMWA MOTO NA BOSI WAKE SAA 32 ZA MATESO

DAR ES SALAAM: Odemali Henry (28), mkazi wa Buguruni jijini Dar es Salaam, amepitia mateso makali ya saa 32 baada ya kudai kuchomwa moto na bosi wake aliyemtaja kwa jina moja la Methew, mkazi wa Temeke jijini Dar.

Kwa mujibu wa mashuhuda, tukio hilo lilijiri hivi karibuni, majira ya saa 5:00 usiku, maeneo ya Buguruni- Rozana, Dar baada ya Odemali kushindwa kumpelekea bosi wake huyo pesa za makusanyo ya wiki ya bodaboda.

Kwa mujibu wa Odemali, bosi wake huyo alimbeba na kumtupa kwenye moto uliokuwa unachoma takataka pembeni mwa barabara na kumsababishia kuungua sehemu mbalimbali za mwili na kupata maumivu makali.

ODEMALI ASIMULIA

Akizungumza kwa tabu na gazeti hili huku akiwa na maumivu makali akiwa nyumbani kwake baada ya kutoka hospitalini, Odemali alisema alifanyiwa unyama huo baada ya kutokuwa na pesa za kumpa bosi wake huyo.

“Ni kweli bosi wangu alinipa pikipiki yake nikawa ninaifanyia biashara ya kusafirisha abiria.

“Nilikuwa sijamaliza hata mwezi mmoja tangu aliponipa kwa makubaliano maalum, sasa nilikuwa nimekosa hesabu ya kumpa ndipo akanipigia simu akaniuliza vipi kuhusu pesa? “Nilimwambia ngoja nije tuonane, akaniambia sawa.

WAONANA, WAONGEA

“Ndipo nikaonana naye, nikaongea naye, nikamwambia mambo yamekaa vibaya, naomba nikuone siku inayofuata, akaniambia yeye ana shida na hizo pesa, nikaendelea kumwambia kuwa mambo siyo mazuri, sina pesa na nikamuomba tuonane siku inayofuata.

“Wakati ninaongea naye alitokea kaka mmoja, akawa ananiita, nikamwambia yule bosi wangu ngoja niongee na huyo jamaa aliyeniita halafu nakuja, akaniambia ngoja tumalizane kwanza.“Mimi nilimwambia nilishakwambia kuwa kwa leo sina pesa, tutaonana siku inayofuata, akaniambia hayo hayamhuhusu.

“Niliendelea kumuomba kuwa tutaonana kesho yake, lakini alikaa kimya. “Baada ya hapo nilimwacha yule bosi wangu, nikaenda kuongea na yule jamaa aliyeniita baada ya kufikiri kuwa bosi wangu amenielewa. “Baada ya hapo nilikwenda dukani, nikanunua soda, nikawa narudi nyumbani kwa kuwa muda huo nilikuwa nimeshapaki pikipiki.

BOSI AMFUATA

“Nikiwa njiani kuelekea nyumbani, kuna uchochoro nilipita, yule bosi wangu akanifuata kwa kasi, akaniambia hatujaelewana. “Niligeuka nikamfuata, akaniambia mbona ninaondoka wakati sijampa uhakika? Nikamwambia nilimwambia nitamuona kesho yake.

“Wakati tukiongea aliniambia nimfuate tukaongee gereji, sehemu ambayo ninapaki pikipiki, nikafikiria labda tunaenda gereji ili aniambie nimpe pikipiki yake. “Wakati tukielekea gereji kuna sehemu kuna mfereji na kulikuwa na watu walikuwa wanachoma takataka, ile tunafika karibu na moto, nilishangaa bosi wangu akinibeba na kunitupa motoni.

MAUMIVU ZAIDI

“Kilichonisababishia maumivu zaidi nilipokuwa nataka kunyanyuka alinikanyagia pale kwenye moto. “Alipokuwa akinifanyia hivyo, kulikuwa na watu watatu waliokuwa pembeni, wakashtuka na kuja kunivuta huku nikipiga kelele za maumivu zilizosababisha watu wengine kuja kunishuhudia.

“Nakumbuka kuna dada mmoja alikimbia kutafuta asali na kuja kunipaka ndipo wengine wakaleta pikipiki wakanibeba na kunipeleka Kituo cha Polisi cha Buguruni.

APELEKWA HOSPITALINI

“Pale Polisi Buguruni, maaskari walinipakia kwenye defenda wakanipeleka Hospitali ya Amana. “Baada ya hapo mama yake na huyo bosi wangu alipewa taarifa, akaja hospitalini na kusema atanisaidia katika matibabu, lakini siku ya pili alipopigiwa simu alisema yeye hana pesa tuazime mahali atarudisha. Siku ya tatu ikawa kimya mpaka mwisho na hata kwenye simu akawa hapatikani tena.

JALADA LA KESI

“Kwa hiyo ndugu zangu ndiyo ambao wananisaidia gharama za matibabu, nasikia bosi mwenyewe alikamatwa, sasa yupo Kituo cha Polisi cha Buguruni (Dar) na atafikishwa mahakamani muda wowote baada ya kufunguliwa jalada la kesi namba BUG/RB/8399/018 -KUJERUHI.

“Kiukweli baada ya tukio lile zilipita kama saa 32 (siku moja na saa nane) za maumivu makali na mateso ambayo sijawahi kuyapitia. “Usiombe upate majeraha ya moto, yanauma mpaka basi,” alisimulia Odemali kwa uchungu.

KAMANDA ILALA

Baada ya kumsikia jamaa huyo, gazeti hili la Risasi Jumamosi lilimtafuta Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, ACP Salum Hamdani ili kuthibitisha kama kweli jambo hilo lilifika mezani kwake ambapo alikuwa na haya ya kusema: “Taarifa juu ya tukio hilo sina kwa sababu ndiyo nimerudi kazini baada ya likizo ya dharura ila nitafuatilia kama kweli tukio hilo limefika ofisini kwangu.”

 Said Ally, Dar es Salaam

UCHAWI!! MANARA Amlipua Ajibu Imani za Kishirikina

Comments are closed.