ALIYEDAIWA KUUAWA NA MUMEWE AZIKWA NA SANDA NYEUSI

MAAJABU! Sintofahamu imeibuka kwa wakazi wa Mtaa wa Pombo-Madale, nje kidogo ya Jiji la Dar katika mazishi ya marehemu Rose Charles.  

 

Rose alidaiwa kuuawa na mumewe, Bakari Mselemu Usama, siku ya Januari Mosi, mwaka huu walipokuwa wakisherehekea mwaka mpya baada ya kutokea kutokuelewana kati yao. Mazishi hayo yalifanyika maeneo hayo ya Pombo, katikati ya wiki hii ambapo katika hali ya kustaajabisha marehemu huyo alizikwa na sanda nyeusi, tofauti na ilivyozoeleka ambapo sanda huwa ni nyeupe.

 

Mbali na hilo, pia suala lingine lililostaajabisha ni kitendo cha msalaba kuwekwa upande wa miguuni kwenye kaburi badala ya kichwani hivyo kuibua hisia za ushirikina. Risasi Jumamosi lilizungumza na familia ya Rose juu ya kile kilichotokea kwenye mazishi hayo ya ndugu yao na kwamba kilikuwa na tafsiri gani.

 

Mugabe Atanasi ni kaka wa marehemu Rose ambaye alilieleza gazeti hili kuwa  siyo ushirikina bali ni utaratibu tu katika mila zao kama Wamakonde kufanya hivyo ingawa hakuna ndugu yao yeyote aliyewahi kuzikwa kwa staili hiyo. “Sisi katika mila zetu ni kwamba dada yangu ameuawa. Ni kama amekufa kwenye vita, hakuugua na wala hakufa kwenye kifo cha kawaida.

 

“Ndiyo maana tulizika kwa staili hiyo. Ni kweli kabisa tulimvisha sanda nyeusi na msalaba tuliuweka miguuni badala ya kichwani. “Nashindwa hata kuzungumza kutokana na tukio alilofanyiwa dada yangu maana ilinibidi nimuangalie jinsi alivyoumia alipofanyiwa upasuaji kwa ajili ya uchunguzi. Tulimuomba daktari tuone, tulichokiona, kile kisu cha kwenye titi kiliingia hadi kwenye moyo, kikautoboa.

 

“Jeraha lililosababisha afe  ni lile la sehemu za siri maana nyama zilitoka nje. “Ulikuwa ni uuaji wa kutisha. Huwa tunausikia tu kwa watu, lakini usiombe yatokee katika familia yako. “Yule shemeji yangu, kama alishindwana na dada yangu ni bora angemrudisha nyumbani maana siyo mara ya kwanza wao kugombana kuliko tendo la kinyama alilomfanyia. “Naomba Serikali iingilie kati suala hili kwa nguvu zote ili mtuhumiwa akamatwe na kuchukuliwa hatua zinazostahili,” alisema Mugabe kwa uchungu.

Mmoja wa mashuhuda ambaye hakutaka jina liandikwe gazetini alisema hajawahi kuona marehemu akizikwa na sanda nyeusi hivyo akawa anahisi kuna ushirikina ndani yake. “Sijawahi kuona marehemu akizikwa na sanda nyeusi na msalaba kuwekwa kwenye miguu badala ya kichwani nimeshangazwa sana.

 

“Pale makaburini kulikuwa na wachungaji, nafikiri ni wa kanisa la kilokole. “Baada ya kufanya ibada fupi waliondoka, lakini familia ilibaki, ikafanya hivyo, ilibidi tubaki na mshangao. “Sasa hivi watu hata usiku hawatoki kwenda msalani, wameingiwa na woga kutokana na tukio hilo, halafu cha ajabu, mtuhumiwa anaonekana usiku.

 

“Kuna siku mtu mmoja alikutana naye saa saba usiku akiwa amevaa sketi ndiyo maana kila mtu amekuwa muoga na amani imetoweka kabisa. “Tunaiomba Serikali itusaidie aweze kukamatwa maana ni mzaliwa wa hapa, akitembea labda ataishia Kibaha tu, hawezi kufika mbali hivyo kumkamata ni rahisi,” alisema mmoja wa mashuhuda hao.

STORI: Neema Adrian, DAR ES SALAAM

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Loading...

Toa comment