The House of Favourite Newspapers

 Aliyeisumbua Zesco arejea Yanga

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mkongomani, Mwinyi Zahera, amemjumuisha kiraka wake Mapinduzi Balama kwenye msafara wa timu hiyo utakaoifuata Zesco Zambia.

Yanga inatarajiwa kuvaana na Zesco Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa huko Ndola, Zambia.

 

Awali, ilielezwa kuwa kiraka huyo anayemudu kucheza nafasi za kiungo na beki wa pembeni namba mbili, hatakuwepo katika msafara utakaoelekea Zambia leo Jumanne saa 2:00 usiku kutokana na maumivu ya paja aliyoyapata kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Zesco, Uwanja wa Taifa. Hakumaliza mchezo huo, alitolewa kipindi cha pili akaingia Ally Ally.

 

Sasa mashabiki wa Yanga wanatakiwa wapate matumaini kwani kiungo huyo atakuwepo katika mchezo huo wa pili wa Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambao Yanga wanatakiwa wapate bao ili wasonge mbele baada ya sare ya 1-1 jijini Dar.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema kuwa Mapinduzi anaendelea vizuri baada ya kumaliza matatibu yake ya wiki mbili akiuguza maumivu ya paja.

Saleh alisema kuwa kiraka huyo wiki hii anatarajiwa kuanza mazoezi magumu pamoja na timu hiyo itakapofika Zambia itakapokwenda kuweka kambi ya maandalizi ya mchezo huo.

 

Aliongeza kuwa kiungo hiyo alipewa wiki mbili za matibabu na mapumziko kwa hofu ya kujitonesha ili mchezo ujao dhidi ya Zesco awepo uwanjani tayari kwa pambano hilo.

“Balama ni kati ya wachezaji watakaokuwepo kwenye msafara wa timu yetu itakayoifuata Zesco kucheza mchezo wa marudiano.

 

“Hiyo ni baada ya kumaliza matibabu na mapumziko ya wiki mbili ambayo alipewa na daktari ambayo rasmi yalimalizika Ijumaa iliyopita, hivyo wiki hii ataanza mazoezi ya pamoja na wenzake kujiandaa na mchezo dhidi ya Zesco.

 

“Mchezo huo ni muhimu kwetu kupata ushindi, hivyo kocha amepanga kumtumia Balama baada ya Boxer (Paul Godfrey) kuwa nje ya uwanja kutokana na majeraha,” alisema Saleh.

Comments are closed.