The House of Favourite Newspapers

ALIYEKUFA AJALI YA MWENDOKASI MAPYA YAIBUKA!

KILOSA: Moja ya ajali mbaya zilizotokea katika msimu huu wa Sikukuu ya Pasaka ni pamoja na ile iliyotekea siku ya Ijumaa Kuu maeneo ya Magomeni-Mapipa jijini Dar iliyohusisha gari ndogo aina ya Nissan March lenye namba za usajili T 968 DNZ na basi la mwendokasi. 

 

Katika ajali hiyo, dereva wa gari ndogo linalofanya biashara ya Ubber aliyefahamika kwa jina la Abdallah Shaban Mbalinyi alfariki dunia hapohapo huku gari lake likiachwa likiwa nyang’any’anga.

 

AJALI ILIVYOKUWA

Inaelezwa na mashuhuda kuwa, Abdallah alikuwa akikata kona maeneo ya Magomeni akitokea Kariakoo kuelekea Kinondoni na wakati anataka kukata kona katika taa ndogo za kuongoza magari za Magomeni-Mapipa ambazo zilikuwa haziwaki kwa wakati huo, gari lake likachelewa kupita na hapo ndipo basi la mwendokasi lilipomvaa na kusababisha ajali hiyo mbaya iliyoondoa uhai wa jamaa huyo.

 

“Baada ya mwendokasi kumpitia, gari ndogo lilikatwa katikati na hapo hapo jamaa huyo akafariki dunia, yaani ilikuwa ajali mbaya kwa kweli kuwahi kuishuhudia kwa macho yangu,” alisema Juma Kassim ‘JK’.

Mwingine aliyefahamika kwa jina la Saida Humud aliliambia Uwazi: “Ni kama kifo kilikuwa kinamuita maana nilimuona tangu akitokea Kariakoo, nilishangaa kuona tu tayari ajali imetokea na nilipokaribia nikakuta ameshakufa. Yaani nilishindwa kuamini macho yangu.”

MAPYA YAIBUKA!

Kufuatia ajali hiyo mbaya, Gazeti la Uwazi lilifuatilia kwa karibu na kubaini kuwa Abdallah alikuwa akiishi Mbagala jijini Dar na ndiko alikokuwa akifanyia biashara zake na siku ya tukio alikuwa akitoka Kariakoo kuelekea Kinondoni kwenda kumchukua dada yake bila kujulikana alikuwa akimpeleka wapi.

 

Akizungmza na Uwazi, mmoja wa marafiki wa karibu wa Abdallah aliyejitambulisha kwa jina la Johnson alisema, siku ya tukio, wakati anawaaga kwenda Kinondoni, walishakubaliana kuwa Siku ya Sikukuu ya Pasaka wangeisherehekea kwa aina tofauti.

 

“Siku ile ya ajali asubuhi yake tukiwa kijiweni Abdallah ambaye sisi tulikuwa tukimuita Ukawa alionekana kuwa muongeaji sana tofauti na siku nyingine. Akawa anatuambia kuwa, Siku ya Pasaka anataka tufurahi na atatufanyia bonge la sapraizi, nimeshangaa na kushtuka baadaye kuja kuambiwa eti jamaa kafariki dunia,” alisema Johnson huku akilengwa na machozi.

UWAZI MSIBANI

Gazeti hili la Uwazi lilifanikiwa kufika Kilosa mkoani Morogoro kuhudhuria mazishi ya Abdallah ambapo huko nako yaliibuka mapya baada ya mmoja wa ndugu zake kueleza kuwa, kifo hicho kilitokea wakati jamaa huyo akihangaika kumtibia dada yake aliyekuwa akiumwa.

 

“Yaani kila kitu Mungu ndiye anayepanga. Abdallah siku ile ya ajali alikuwa akienda Kinondoni kumchukua dada yake aliyekuwa akiumwa siriasi ili ampeleke Hospitali ya Muhimbili. “Sasa, kabla ya kutimiza lile alilokuwa anataka kulifanya, Mungu akamchukua. Sisi hatuna la kufanya zaidi ya kumuombea huko aliko Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi,” alisema ndugu huyo.

Licha ya Uwazi kufanikiwa kumuona mke wa marehemu aliyefahamika kwa jina la Fatina Hassan ambaye aliliza wengi msibani, akiwa kwenye hali mbaya kufuatia msiba huo wa ghafla, halikufanikiwa kuzungumza naye. Abdallah alizikwa kwao Kilosa mkoani Morogoro Jumapili iliyopita na ameacha mke mmoja na watoto watano ambao ni Shabani, Sikudhani, Sabrina, Amani na Karim Mbilinyi.

 

Gazeti hili linatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki na linawaombea kwa Mungu awape nguvu katika kipindi hiki kigumu. Inna Lillah Wainna Ilaih Rajiun.

Comments are closed.