ALIYEMUUA MKE, MKWE, JIRANI… UNDANI WAANIKWA

MOROGORO: Tukio la Michael John Mwandu, mkazi wa Dumila, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro la kumuua mkewe, jirani na mkwewe na kisha naye kujiua bado limeendelea kuwa gumzo na Amani limefika eneo la tukio na kukuletea undani wake.

 

Mwandu alidaiwa kufanya unyama huo Mei 25, mwaka huu huku chanzo cha mauaji hayo kikiwa ni wivu wa mapenzi. Mwandishi wetu baada ya kupata taarifa za mauaji hayo ya kutisha, alipiga gia bodaboda yake na kutinga eneo la tukio umbali wa kilometa 70 kutoka Morogoro Mjini.

 

ALICHOSHUHUDIA

Alipofika alishuhudia maiti za watu hao zikiwa zimesambaa kwenye vichaka vya mtaa huo huku kundi kubwa la watu wakijitokeza kuzishuhudia.

 

Baadaye polisi wa Kituo cha Polisi Dumila walifika eneo la tukio na kuchukua maiti hizo na kwenda kuzihifadhi. Baada ya taratibu hizo za kipolisi kukamilika huku mwandishi wetu akipiga picha kwa hatua, alipata nafasi ya kuwahoji watu mbalimbali akiwemo mke mkubwa wa muuaji huyo, majirani na mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo.

TUANZE NA MWENYEKITI

Mwenyekiti huyo, Jackson Senyagwa alianza kwa kuthibitisha kutokea kwa mauaji hayo kisha kueleza jinsi ilivyokuwa siku ya tukio.

 

“Ni kweli mauaji hayo yanayohusishwa na wivu wa mapenzi yametokea hapa mtaani kwa Michael John Mwandu kumuua mkewe mdogo aliyekuwa na ujauzito kwa kumnywesha sumu kisha kumfungia ndani na kwenda chumba cha pili anachoishi mama mkwe wake na kumuua kwa kumkatakata mapanga,” alisema Senyagwa.

AMUUA JIRANI

Akizidi kusimulia tukio hilo la kikatili, mwenyekiti huyo alisema baada ya kumuua mama mkwe wake, alikwenda kwa jirani ambaye ni rafiki wa marehemu mkewe.

 

“Kisha akaenda kwa rafiki wa mkewe na kumuua pia kwa kumkata mapanga baadaye akarudi kwake na kujiua kwa kunywa sumu ambayo inadhaniwa kuwa ni dawa ya mimea,” alisema mwenyekiti huyo.

 

TUMSIKILIZE MKE MKUBWA

Naye mke mkubwa wa Mwandu, Mwajuma Mohamed (40) alipotakiwa kuelezea tukio hilo alisema: “Siku ya tukio ilikuwa zamu ya mume wangu kwenda kulala kwa mke mdogo aliyekuwa anakaa na mama yake mzazi, cha ajabu asubuhi nikapokea taarifa kwamba mume wangu niliyezaa naye watoto wawili, Lea na Tadeo amemuua mke mwenzangu na mama mkwe wake kisha akamuua rafiki wa mke wake na yeye kujiua.

 

ALIWAHI KULALAMIKA

“Siku za nyuma alilalamika kwamba mkewe huyo mdogo aliyemkuta na mtoto mmoja hakuwa mwaminifu kwenye mahusiano yao mimi sikuingilia wakawa wanamalizana wenyewe hadi lilipotokea tukio hili la mauaji,” alisema mke huyo mkubwa wa Mwandu ambaye kwa mujibu wa maelezo yake licha ya kuishi na mumewe huyo kwa miaka mingi hawakufunga ndoa kwa sababu za utofauti wa dini pia mama huyo alisema hata huyo mke mdogo pia hawakufunga naye ndoa.

 

MAZISHI

Licha tukio hilo kutokea Mei 25, mwaka huu, maiti zote zilizikwa isipokuwa ya Mwandu ambapo hadi juzi Jumanne ilikuwa bado haijazikwa licha ya wanandugu kukabidhiwa maiti hiyo.

 

HALI ILIVYOKUWA MSIBANI

Jumanne, mwandishi wetu alitinga tena eneo la msiba nyumbani kwa mke mkubwa wa Mwandu na kushuhudia watu wachache, wengi wao wakiwa ni wanandugu huku majirani wakionekana kususia msiba huo wakimshutumu marehemu huyo kuwauwa wenzake bila hatia. Kufuatia hali hiyo mwandishi wetu alizungumza na baadhi ya majirani ambao walikubali kuzungumza kwa sharti la kutotaja majina yao gazetini.

 

“Mwandu ni jirani yetu lakini kwa hili alilolifanya kuuwa watu akiwemo mkewe mwenye kiumbe tumboni ni dhambi kubwa hivyo kuomboleza au kushiriki mazishi yake sisi majirani tunaona kama tunafurahi kwa hilo alilolifanya. Sisi tunafanya hivi ili kuonyesha kwamba tumechukizwa, tumeamua kutokanyaga kwenye msiba wake. “Ndugu zake wenyewe wanasinyaa kumzika, maiti zote zimekabidhiwa isipokuwa ya muuaji tu.”

 

TUJIKUMBUSHE

Hili ni tukio la pili kutokea kwenye mtaa huo ndani ya kipindi cha takriban miezi miwili ambapo tukio la kwanza, mganga wa kienyeji alimuua mkewe mdogo aliyekuwa na mtoto mchanga kisha na yeye akajiua chanzo cha mauaji hayo kikiwa ni hicho hicho cha wivu wa mapenzi. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Willbroad Mutafungwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo kwenye mkoa wake na kueleza kuwa limetokana na wivu wa kimapenzi.


Loading...

Toa comment