The House of Favourite Newspapers

ALIYEPASULIWA KICHWA BADALA YA MGUU… MIL. 100 ZAMTESA

KIJANA mmoja Emmanuel Di­das Marishay (30) mkazi wa Kigogo, jijini Dar es Salaam ambaye alipasuliwa kichwa badala ya mguu, shilingi milioni mia moja alizoahidiwa kupewa zinamtesa kwani amekuwa akiziwaza kila siku na kufikia hatua ya kuzimia mara kwa mara; tatizo linalosababishwa na msongo wa mawazo.  

 

Akizungumza na Ijumaa Wikienda, juzi Jumamosi Em­manuel alisema kuwa ana­muangukia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli ili aweze kulipwa fedha zake hizo kama ilivyoamuriwa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar kwani ndizo zinasababisha yeye kuteseka kila akiyawaza malipo hayo.

 

“Kwa sababu rais amekuwa akisaidia wengi anaamini hata­niacha. Unajua kila nikikaa na­hisi kama sitalipwa hizo pesa kwani kuna gazeti moja liliwahi kuandika kuwa nimelipwa kitendo ambacho kilinisumbua akili yangu mpaka nikafikia hatua ya kulazwa tena Moi ambapo nilikuwa nikisum­buliwa na maumivu ya kichwa hadi nimerudiwa na ugonjwa wa kuanguka mara kwa mara,” alisema Emmanuel.

 

Aidha, alisema kuwa anaiomba serikali kupitia Kitengo cha Mifupa na Mishipa ya Fahamu (Moi) wamlipe fed­ha zake hizo ili aweze kujikimu kimaisha kwa kufanya mambo mengine ya kumuingizia kipato kwani kutokana na masharti aliyopewa hawezi kufanya kazi nyingine ngumu zaidi na ile anayoifanya sasa Moi alipoa­jiriwa baada ya makosa ya upasuaji kufanyika.

 

“Nipo Kitengo cha Moi kikazi ili kujipatia kipato, lakini wakinilipa nitaweza kufanya mambo mengine ya kimaisha kwani nimekatazwa kutembea mwendo mrefu na sasa nina­vyoumwa hivi naona kama ni­tashindwa hata kufanya kazi, nawaomba sana Moi wanilipe kwani kila nikifikiria najikuta nachanganyikiwa,” alisema Emmanuel.

 

ALIFIKAJE HAPA?

Mwaka 2007 Emmanuel alipata ajali ya pikipiki eneo la Magomeni, Dar alipokuwa kwenye mizunguko yake, baa­da ya hapo alilazwa Hospitali Taifa Muhimbili Kitego cha Mifupa na Mishipa ya Fahamu ambapo alipewa matibabu ya awali na ikaonekana kuwa anatakiwa kufanyiwa upasuaji wa mguu ili apone.

MAKOSA ALIYOFANYIWA HOSPITALI

Emmanuel anadai kuwa alipokuwa anaumwa alitakiwa kufanyiwa upasuaji wa mguu lakini kwa bahati mbaya dak­tari aliyepangiwa kumfanyia upasuaji alichanganyiwa mafaili na kum­fanyia upas­uaji wa kichwa badala ya mguu kwani majina ya wagonjwa wali­otakiwa kufanyi­wa upasuaji siku hiyo yalikuwa yakifanana ambapo yeye anaitwa Em­manuel Didas na aliyekuwa na uvimbe kichwani alikuwa akiitwa Emmanuel Mgaya.

 

“Kilichotokea ndani ya chumba cha upasuaji ni kwamba daktari alipofika alikuta nimeshapigwa sindano ya usingizi ndipo akashangaa kuona sijan­yolewa nywele, akaninyoa na kunifanyia upasuji, endapo ningekuwa sijalazwa kwa sindano ningejitetea kwani sikuwa na tatizo lolote la kichwa,” alisema Emmanuel.

 

APELEKWA INDIA

Baada ya kufanyiwa upasuaji kimakosa wa kichwa alipe­lekwa India kwa gharama za Moi ambapo alipewa dawa za kumrejesha katika hali ya kawaida na kumtuliza kichwa ambapo alirudi nchini na kuendelea na maisha.

 

APANDA MAHAKAMA KUU

Baada ya upasuaji huo, Emmanuel alifungua kesi Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, kudai fidia ambapo alishinda kesi hiyo na kutakiwa kulipwa shilingi milioni 100 ambazo mpaka sasa ndizo anazolalamikia kuwa hajalipwa.

 

Jaji Zainabu Muruke ali­yetoa hukumu hiyo alisema Sh. 1,076,620 ni fidia maa­lumu kwa kukosa kipato kwa kipindi cha miezi 21, tangu Novemba Mosi, 2007 ambapo Didas alifanyiwa upasuaji hadi Agosti 24, 2009 alipoajiriwa na Moi kama mhudumu wa karakana. Baada ya kuongea na Emmanuel Gazeti la Ijumaa Wikienda lili­zungumza na Meneja Uhusiano wa Moi, Almas Jumaa juu ya madai hayo ya fedha ambapo aliomba atafutwe Jumatatu (leo) kwani alikuwa katika mapumziko ya wikiendi.

 

“Siwezi kuongea lolote kwa leo naomba uje ofisini siku ya Jumatatu (leo) kwa sababu leo ni wikiendi na sina ‘dokumenti’ yoyote hapa,” alisema Almas. Kutokana na gazeti hili kwenda mtamboni kabla ya Jumatatu kupewa majibu ya Moi, majibu yake endapo yatapatikana yatachapishwa katika toleo lijalo.

Comments are closed.